
Mwili wa mwanasiasa mkongwe nchini Kenya Raila Odinga, umewasili huko Bondo karibu na kaunti ya Siaya tayari kwa mazishi ya faragha yatakayofanyika siku ya Jumapili. Kabla ya kufikishwa Bondo, mwili wa Odinga uliagwa na umati mkubwa wa waombolezaji ulijitokeza katika mji wa magharibi mwa Kenya, Kisumu. Watu kadhaa walijeruhiwa wakati wa maombolezo ya Kisumu.
Raila Odinga, aliyekuwa na umri wa miaka 80, alifariki Jumatano nchini India kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa mshtuko wa moyo, na kusababisha majonzi makubwa kote nchini, hasa katika eneo la magharibi mwa Kenya.
Odinga alikuwa kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi wa kizazi chake nchini Kenya. Alihudumu kama Waziri Mkuu kati ya 2008 na 2013, ingawa hakuwahi kufanikiwa kushinda urais licha ya kujaribu mara tano. Kifo chake kimeacha pengo la uongozi katika upinzani nchini Kenya.