
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amewaomba wananchi mkoani humo kutoshawishiwa na yeyote kutumia siku ya uchaguzi mkuu kujifunza kufanya vurugu, badala yake wadumishe amani na utulivu.
Hadi sasa zimebaki siku 12 pekee Watanzania kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi upande wa madiwani, wabunge, wawakilishi na Rais, tukio litakalofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Oktoba 18, 2025 wakati wa mazoezi ya afya ya viungo ‘Jogging’, iliyoandaliwa na klabu ya Jogging jijini humo, Malisa amesema wananchi watumie siku ya uchaguzi kutekeleza haki yao kwa amani kama ilivyo dhima ya mkoa huo.
Amesema wananchi wasikubali kumsikiliza mtu anachokitaka na kufanya siku hiyo kujifunza kufanya vurugu, akieleza kuwa matarajio ni kuona tukio hilo linafanyika kwa amani.
“Twende kufanya kwa amani na utulivu, tusikubali mtu yeyote anachokitaka tujifunze kufanya vurugu, tunataka chaguzi salama,” amesema Malisa na kuongeza:
“Mazingira salama huleta afya bora, tuwapongeze klabu hii kwa mazoezi haya yanayoimarisha afya na kuhamasisha utunzaji mazingira,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wake, muuguzi katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya, Joyce Komba amesema serikali inaingia gharama kubwa kuhudumia wananchi hasa wenye magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.
Amesema magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, moyo na kansa hutokana na kutoushughulisha mwili kutokana na kuishi maisha ya kuiga na kufanya mwili kubweteka.
“Unapofanya mazoezi unasaidia hata mmeng’enyo wa chakula uende vizuri, afya inakuwa salama na mwili kuwa na nguvu, kwa sasa serikali inaingia gharama kubwa kuhudumia wananchi hasa wenye magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza,” amesema Joyce.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Jogging, Abou Mtoro amesema lengo la mazoezi hayo ni kuhamasisha uchaguzi salama akieleza kuwa wao kama wanamichezo wanaungana na Watanzania wote kushiriki uchaguzi mkuu.
“Kaulimbiu yetu ni afya bora, ‘Mazingira safi na uchaguzi salama’, lakini tunahamasisha Uchaguzi salama na kutimiza haki yetu kikatiba kupiga kura, niwaombe Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29,” amesema Mtoro.
Mmoja wa washiri wa mazoezi hayo, Anna Mwaisamila amesema wao vijana ndio kundi maalumu katika kushiriki kutunza mazingira pamoja na kupiga kura.
“Vijana tunahamasishana kulinda na kutunza mazingira, lakini kushiriki uchaguzi salama na matarajio yetu ni kutimiza haki yetu kupiga kura Oktoba 29,” amesema Anna.
Mwenyekiti wa kundi la jogging kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya, Dk Abdallah Njama amesema ili kutimiza majukumu yote inahitajika afya hivyo hamasa iwepo kwa watu kufanya mazoezi.
“Tuwashukuru chama cha Jogging Mbeya Mjini kwa tukio hili lililoambatana na kaulimbiu ya afya, mazingira na uchaguzi salama, yote haya yanaunganishwa na afya,” amesema Dk Njama.