Rais Donald Trump wa Marekani ameionyesha Israel taa ya kijani ili ianzishe tena vita katika Ukanda wa Gaza.

Rais Donald Trump wa Marekani ameionyesha Israel taa ya kijani kwa kisingizio kwamba Hamas haiheshimu makubaliano ya kusitisha vita siku tatu baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani ya Gaza na kuachiwa huru mateka wa Israel. Jumatano iliyopita Trump alisema kuwa  wanajeshi wa Israel wanaweza kuanzisha tena vita huko Gaza ikiwa Hamas haitaheshimu makubaliano hayo. 

Rais wa Marekani amekwenda sambamba na Israel kwa kukariri madai kwamba Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) haitaki kuheshimu vipengee vya makubaliano ya kusimamisha vita Gaza na  hivyo kuitishia harakati hiyo na wakazi wa Gaza kwamba:  “Israel itarejea katika mitaa ya ukanda huo mara tu atakapoamuru.” Ikiwa Israel inaweza kuingia na kuwaponda vibaya sana, itafanya hivyo.” Rais wa Marekani alidai kuwa: “Kinachoendelea kwa Hamas kitarekebishwa haraka iwezekanavyo.”

Licha ya vitisho vyote hivi, Trump aidha amesema kuwa: “vita imekwisha, vita imekwisha, vita imekwisha… unaelewa?!”; matamshi ambayo yanadhihirisha namna misimamo ya Trump inavyokinzana na huwenda aliropoka hayo ili kudhibiti fikra za waliowengi duniani au mashinikizo ya kisiasa dhidi yake.

Trump amebwabwaja hayo huku Israel ikiituhumu harakati ya Hamas kuwa haiheshimu mapatano ya kuwaachia huru na kuwakabidhi metaka wa utawala huo waliokufa na walio hai kama sehemu ya makubaliano ya sitisha vita vita huko Gaza. Viongozi wa Israel wameufahamisha Umoja wa Mataifa kuwa shehena za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza itapungua au kuchelewesha kutokana na idadi ndogo ya miili ya mateka wa utawala wa Kizayuni walioaga dunia. Hata hivyo hadi sasa usitishaji vita huu unaolegalega umedumishwa.  

Inaonekana kuwa, baada ya kukabidhiwa wafungwa wote walio hai wa Kizayuni, Israel hivi sasa imeazimia kwa mara nyingine tena kuwasha moto wa vita katika Ukanda wa Gaza kwa kisingizio kuwa Hamas imeshindwa kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita, na kwa kwamba haijakabidhi maiti za wafungwa wote wa Kizayuni waliokufa. Katika upande mwingine, mawaziri wenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni kama Smotrich na Ben-Gvir ambao wanapinga makubalino ya kusitisha vita Gaza bado hawajajitoa katika serikali ya mseto ya Netanyahu. Inaonekana kuwa mawaziri hao wanasubiri kuvunjika mazungumzo ili waweze kutumia suala hilo kama kisingizio cha kuendelezwa vita. 

Itamar Ben Gvir na Smotrich Bezalel 

Tovuti ya habari ya Axios ya nchini Marekani imeripoti kuhusiana na hili kwamba utawala wa Kizayuni umeitahadharisha Marekani na kutangaza kuwa makubaliano ya kusimamisha vita Gaza yatasitishwa iwapo Hamas haitarejesha miili ya wanajeshi metaka walioaga dunia. Hata hivyo harakati ya Muqawama ya Hamas kwa upande wake inasema kuwa haina miili yoyote ya wanajeshi wa Israel. Viongozi wa Israel wamekiri kuwa itakuwa vigumu kupata miili michache ya wanajeshi walioaga dunia hata hivyo wanadai kuwa kati ya miili 15 na 20 inaweza kurejeshwa haraka iwezekanavyo. 

Marekani kwa upande wake inadai kuwa ina mpango wa kuanza mazungumzo kuhusu awamu inayofuata ya makubaliano hayo, kushughulikia masuala nyeti kama vile nani atatawala Gaza na kudhamini usalama. Viongozi wa Marekani wametangaza kuwa Washington iko katika mazungumzo na nchi 5 na inaanda utaratibu wa kutuma Gaza kikosi cha usalama cha kimataifa. Hata hivyo viongozi wa Israel wametahadharisha kuwa kupiga hatua kuelekea marhaha inayofuata itakuwa vigumu sana bila ya kujulikana hatima ya miili ya mateka wa Kizayuni. 

Inaonekana kuwa  hali ya usitishaji hivi sasa katika Ukanda wa Gaza inalegalega; na kuna kila uwezekano wa kuanza tena mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo. Hasa ikizingatiwa kuwa Netanyahu ana hamu kubwa ya kukiuka makubaliano ya kusimamisha vita na kuanzisha tena mashambulidi dhidi ya Gaza ili kufanikisha malengo yake makubwa ya kisiasa na pia kukidhi matakwa ya mawaziri wenye misimamo ya kufurutu ada wa baraza lake la mawaziri. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *