
Mufindi. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Abdul Abdarahmani amewataka viongozi na watumishi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) kuongeza uwajibikaji katika utekekezaji wa miradi ya maji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili thamani ya miradi hiyo ionekane.
Abdarahman ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 wakati akiwasilisha mada ya Kanuni za Maadili ya Utendaji kwa Utumishi wa Umma na wajibu wa kila mtoa huduma katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Mada hiyo imetolewa kwenye kikao cha robo mwaka kilichowakutanisha wadau wa maji kutoka Mkoa wa Iringa na kufanyika kwenye ukumbi wa NFS, uliopo katika Halmashauri ya Mji Mafinga wilayani hapa.
Abdarahmani amesema Ruwasa, wenyeviti wa bodi na viongozi wa jumuiya za watumia maji (CBWSO) kutoka Wilaya ya Mufindi, Kilolo na Iringa Mjini, wanapaswa kujiepusha na mgongano wa kimaslahi ili thamani ya fedha za miradi zionekane na kulinda hadhi na heshima ya Serikali wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Pia, amesema usimamizi dhaifu wa matumizi ya fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo unaweza kusababisha miradi isiyo na ubora, kwa kuwapata wakandarasi wasio na sifa, hali inayosababisha miradi hiyo kutoa huduma duni kutokana na kushindwa kukamilika kwa wakati.
“Maji hayana mbadala, ndio maana Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji ili wananchi wapate huduma bora, kinyume chake wananchi wanakosa imani kwa watumishi na Serikali yao, hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi mkubwa,” amesisitiza Abdarahmani.
Kwa upande mwingine, amewakumbusha wadau hao kujiepusha na tabia ya kuomba na kupokea rushwa kama kigezo cha mwananchi kupata huduma kwani tabia hiyo inafedhehesha uhalali na taaluma zao.
Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Tupa William amemshukuru Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Mufindi huku akiahidi kuendelea kuishirikisha na Taasisi hiyo kwenye usimamizi wa miradi ya maji mkoani humo ili kuongeza uwajibikaji na usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maji.
” tunashukuru katika kikao hiki tulikuwa na Takukuru kwa ajili ya kutukumbusha wajibu wetu na kutuasa kufanya kazi zetu katika misingi ya maadili ambayo yamekusudiwa na Serikali ili huduma zipatikane kwa njia nzuri kwa wananchi,” amesema Mhandisi William.