
Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kuwa, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, serikali ya Madrid itadumisha vikwazo vyake vya silaha dhidi ya Israel.
Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania amesisitiza kuwa, vikwazo vya silaha vya nchi yake dhidi ya Israel vitasalia licha ya kuweko makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza.
Kulingana na Pars Today, Waziri Mkuu wa Uhispania alisisitiza: “Sasa tuna usitishaji vita, lakini bado tunapaswa kufanya amani.” Amesema, fursa ya kusitisha vita imetokea lakini lazima tushikamane na msimamo wtu huu kutoka Uhispania na Ulaya. Sánchez pia alitangaza utayarifu wa Madrid wa kutuma wanajeshi Gaza kama sehemu ya ujumbe wa kimataifa wa kulinda amani.
Wiki iliyopita pia Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania alisisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha vita Gaza yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Israel yasifanywe kuwa fidia ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel Ukanda wa Gaza.
Uhispania ambayo ni miongoni mwa nchi wakosoaji wakubwa wa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza Septemba mwaka huu ilitangaza kuwa mwendesha mashtaka wa nchi hiyo kwa kushirikiana na mahakama ya ICC atachunguza “ukiukwaji mkubwa” wa haki za binadamu uliofanywa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa uratibu na ICC.