
Umoja wa Mataifa umelaani vikali hatua ya jeshi la Madagascar kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo baada ya maandamano yaliyokuwa yakiishinikiza serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Andry Rajoelina.
Tamko hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye amelaani mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Madagascar baada ya wiki kadhaa za maandamano ya umma dhidi ya utawala wa Rais Andry Rajoelina. Guterres amekosoa mabadiliko ya uongozi yasiyozingatia katiba na ametoa mwito wa kurejea kwa utawala wa kiraia nchini Madagascar chini ya msingi wa katiba. Karipio hilo la Umoja wa Mataifa linatolewa katika hali ambayo, Kanali Michael Randrianirina jana aliapishwa kuwa Rais wa mpya wa Jamhuri ya Madagascar huko Antananarivo.
Tukio hili linakuja siku tatu baada ya Bunge la taifa kumuondoa Mkuu wa Nchi Andry Rajoelina na mamlaka kuchukuliwa na jeshi. Hii inaashiria hatua mpya katika misukosuko ambayo imeitikisa Madagascar tangu kuanza kwa vuguvugu kubwa la maandamano ya kijamii lililoanza Septemba 25, 2025.
Kanali Michael Randrianirina ametakiwa na Mahakama ya Katiba kuitisha uchaguzi ndani ya siku 60 kwa mujibu wa siku atakayoamua, ikinukuu Kifungu cha 53 cha Katiba, ambacho kinahitaji uchaguzi wa urais ufanyike ndani ya siku 30 hadi 60 baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kutangaza kuwa ofisi hiyo imebaki tupu. Jumuiya ya kimataifa inapinga hatua hiyo na imewataka wadau wote wa Madagascar kutafuta suluhisho la amani linaloheshimu katiba ya nchi hiyo.
Umoja wa Afrika umetengaza kuisimamishia unachama Madagascar “hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa” baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Andry Rajoelina.