
Urusi imeishambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine usiku wa kuamkia jumamosi, mnamo wakati mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na Volodomyr Zelenskyyaliyolenga kumaliza vita yakifanyika Washington.
Urusi imefanya mashambulizi zaidi ya 10 katika eneo la mkoa wa mashariki wa Kharkiv. Karibu vitongoji vyote vya mji vimetatizika huku mamlaka zikijaribu kurejesha umeme baada ya kukagua vituo vilivyolipuliwa.
Gavana wa mkoa wa kusini mashariki mwa Ukraine wa Zaporizhzhya Ivan Fedorov pia ameripoti moto uliotokana na mashambulizi ya Urusi. Wakati huo pia wizara ya ulinzi mjini Moscow imeripoti kuzidungua droni 41 za Ukraine zilizolenga eneo la Urusi na Bahari Nyeusi, pamoja na tatu katika mkoa wa Moscow. Ukraine imekuwa ikijilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi kwa msaada wa nchi za Magharibi kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.