Dar es Salaam. Ni wazi kuwa kila zama na vitabu vyake. Zama hizi siyo zile ambazo wazazi waliichukulia sanaa kama uhuni. Hivi sasa wapo wengi wanaoamini katika sanaa hadi kuwaruhusu watoto wao kutafuta ugali katika sekta hiyo.

Hilo linajionesha katika kundi la Tegeta Kids lenye watoto zaidi ya 27 wanaojishughulisha na dansi. Akizungumza na Mwananchi Veronica Jacob ambaye ni mwanzilishi wa kundi hilo linalotamba baada ya kutokea kwenye video ya Diamond, amesema kundi hilo lilianza kama utani.

“Nina mwanangu anaitwa Magreth alikuwa anapata kipaimara, nikamwambia nitamfanyia sherehe nahitaji watoto wa kucheza kwenye sherehe yake. Nikaenda kuomba watoto kwa wazazi. Nikatafuta mwalimu akawafundisha, ikafika siku ya sherehe wakacheza lakini  tukaamua kuliendeleza kundi ndiyo mpaka leo,” anasema.

“Sasa lina miaka minne inaelekea mitano. Tuna watoto 28 tulianza na watoto  sita. Hata mimi  nilivyokuwa binti, nilikuwa napenda kucheza. Hili kundi siyo la kwanza nilivyokuwa nakaa Mbagala nilianzisha kundi langu tulikuwa tunacheza kwenye maharusi,” anasema mama huyo. 

Walivyopata mchongo kwa Diamond

Kundi la Tegeta Kids ndilo limeipamba video ya ‘Nani’ wimbo wa mwanamuziki wa Bongo Fleva Diamond Platnumz, uliotoka mapema wiki hii.

Veronica anasema walipokea mwaliko wa kutokea kwenye video hiyo bila kujua inamuhusu nyota huyo wa Bongo Fleva.

“Tulikuwa Bagamoyo tukapata simu kutoka kwa maproduza wake.  Mwanzo walituficha wakasema tunatakiwa Tegete Kids waongezeke na wengine wafike 100  ili waweze kufanya video. Siku ya kurekodi msanii alikuwa Zanzibar kwa hiyo ilipelekwa mbele hadi Ijumaa.

“Tuliangalia kwenye mitandao tukawa tunachukua namba za vikundi vingine tukaunganisha wakafika watoto kama 80. Siku ilipofika walinipigia wakasema siku yenyewe ni kesho baada ya kufika kuona mabaunsa nikaamini kweli tunaenda kufanya kazi na Diamond,” anasema. 

Hata hivyo Veronica ameficha kiasi cha malipo walichopokea kwa nyota huyo huku akidai walipatiwa pesa ya kutosha akaifanyia mgao na kila mtoto aliridhika.

“Kiukweli kila ninapopita watu wanasema mimi tajiri, siyo mwenzao na Mage ndiyo kabisa ila tunachosema sisi siyo mastaa ila tunaomba Mungu tufike huko. Zamani tulikuwa tunawaangalia sana Ghetto Kids lakini kwa sasa tunajiamini.

“Tumeshafanya kazi na Konde Boy kwenye wimbo ‘Kidedea’, kuna kipengele cha mazombi pale watoto ndiyo walipafomu. Wengine ni  Chinno na Rayvanny tumefanya clip,” anasema.

Licha ya mafanikio yaliyoanza kujitokeza katika kundi hilo Veronica anasema watu walimkatisha tamaa wengine walidai amekuwa chizi.

“Wakasema mimi ni chizi muda wote nakaa na watoto. Mara  nawafundisha tabia mbaya, kuna wazazi wakawatoa hadi watoto wao. Nilimwambia Mungu anivushe kwa sababu najua kipaji changu.

“Kundi la Tegeta Kids kwanza tunazingatia heshima, mavazi ya ajabu kwa mtoto mdogo hatutaki. Tunaangalia na kuheshimiana wao kwa wao. Kwa sasa kila mtu anaishi kwao muda wa mazoezi ni saa 11 baada ya kutoka shule,” anasema.

Anasema ili mtoto aingie katika kundi hilo ni lazima afuate masharti.

“Kuna watoto wengine wanakuja kuomba wajiunge. Akifika tunamuwekea muziki ajaribu  tukiona anaweza inabidi afuate taratibu  zetu za kujiunga. Kuna fomu na malipo,  passport ya mzazi, aende kwa mjumbe na serikali za mitaa maana kikundi kimesajiliwa Basata hivyo hadi mzazi aridhie.

“Ninachowaambia wazazi hawawezi kujua la kesho  kwa hiyo kama kuna uwezo wa kuleta watoto wakuze vipaji vyao ni sawa.  Watu huwa wanauliza kama watoto wanasoma lakini hapo unavyoona kuna wengine wanatoka shule mazoezini wanakutana jioni,” anasema.

Ikumbukwe Tegeta Kids ndiyo walikuwa washindi wa challenge ya Amanda wimbo wa mwanamuziki Zuchu. Hivyo walifanikiwa kushinda Sh2 milioni.

Huyu hapa mwalimu wa Tegeta Kids

Mbali na mwanzilishi wa kundi hilo Ramadhan Adam  ‘Teacher Tiny’ ambaye  ni mwalimu wa kundi hilo anasema alikuta kundi hilo lina jina jingine hivyo akaanzisha utaratibu mpya.

“Niliwakuta  wakiwa wadogo sana, ndiyo kwanza wameanzisha hili jambo. Baada ya kuwaona wana kitu nikamfuata Bi Mkubwa nikamwambia  kama inawezekana niwashike mkono kwa sababu niliwakuta mazoezini hiyo siku.  

“Nilikuwa napita njia ndiyo nilikutana nao nikajikuta navutiwa nikawa nimesimama, nikawaambia nataka niwafundishe wimbo moja ilikuwa mwaka 2023  niliwawekea wimbo wa Baddest. Niliwafundisha kwa muda mfupi wakashika,” anasema.

Mwalimu huyo anasema hapo ndipo safari yake na kundi hilo ilianza.

“Akasema ameshakuwa na baadhi ya walimu lakini hakuna kitu. Akanitajia jina la kundi kipindi hicho lilikuwa linaitwa ‘Top Town’  nikamwambia  nataka tubadilishe jina tukaanza kujiita Tegeta Kids.  Nilikuwa na akaunti yangu ya Instagram ilikuwa na watu 1000 tukaanza nayo hiyo na upande wa Tiktok tukafungua.

“Baada ya muda tukaanza kupata show, mwisho online wakaanza kuonekana. Nakumbuka video iliyotrendi ni ile ‘Twende DJ Mamama Weee’ ‘Honey’ ya Zuchu  hapo watu kidogo wakaanza  kutufuatilia safari ndiyo ilivyoanza,”anasema  ‘Teacher Tiny’

Diamond Kitambo
“Sisi DM ya kwanza ya Mondi ilikuja kwenye Komasava.  Tulifanya kwa mara ya kwanza challange Mondi aliaccept video. Tulishangilia sana  baada ya ile akatutumia meseji akasema mnafanya vizuri hongereni. Niliscreen short nikatulia nayo nikasema safari bado ndefu. 

“Hatuwezi kujua  tunaweza kuweka mtandaoni akapenda au asipende, tukakaa nayo tukawa tunamtumia meseji nyingi akawa hajibu. Ikatokea siku nimekaa na watoto nikasema namtumia  sms nione kama atajibu  nilivyotuma nikaona amesoma  ilikuwa 2024 mwanzoni.

“Nilikuwa namuomba sapoti, lile jambo lilimgusa akajibu  akasema kiukweli nimewaelewa sana pia mnapokuwa na jambo lolote msisite kusema.  Sasa ile ndiyo ilitushinda  tukaiposti furaha ilituzidi, lakini hata wasanii wengine walikuwa wanatuonesha moyo sana,” anasema Mwalimu.

Mazoezi bila muziki
Mwalimu huyu anasema kitu ambacho anazingatia katika kuwafundisha watoto ni nidhamu ya uchezaji.

“Siku ya kwanza hatukujua kama tunaenda kufanya video ya Diamond, tulitunga staili bila muziki tukasema kama ikiwa Amapiano tutaweka staili hizi tukajua lazima atatengeneza wimbo ambao unachezeka.

“Siku nyingine wakatutumia wimbo tukajua sasa ni Diamond. Nikawaambia wacheze tu lakini huwezi kuamini ni zile video ambazo zinatrendi kwenye behind the scene zinaua sana. Sasa tulivyofika, maneno yalikuwa hayaendani na style kwa sababu sisi tulicheza bila muziki tukaona tutunge nyingine palepale mimi na Mose Iyobo,” anasema.

‘Nani’ ni wimbo uliotoka pamoja na video yake hivyo ili kuepusha uvujishwaji anasema kuna masharti alipewa.

“Niliambiwa nikiwasha muziki usitoke nje na mimi huu ni ugali wangu. Nilikuwa na madensa karibia 100 lakini nilitoa onyo na nikachukua simu zote, muziki haukuwa mkubwa  kwa sababu  nikivujisha wimbo Mondi hawezi kutuelewa na hata future zetu zitakata,” anasema.

Sababu Magreth kulia mbele ya Diamond

Wakati video ya ‘Nani’ inaanza anaonekana binti, jina lake Magreth huyo ndiye anatajwa kuwa sababu ya kundi hilo kwani lilianza siku ya kipaimara chake.

“Sikutegemea kama video inavyoanza mimi ndiyo nitaonekana.  Maana mwanzo aliwekwa mtu mwingine baadaye dairekta akaniita mbele akaniambia nifanye kama alivyofanya yule wa mwanzo.

“Video ilivyotoka sikujua nilikuwa nimelala. Nilivyoamka watu wakanifuata kuwa video imetoka,  muda huo mwalimu akasema twende kwanza kwenye mazoezi kisha tuangalie nilivyoiona nilifurahi sana sikutarajia.

“Nililia siku ambayo tunashoot video kwa sababu kuna maneno alikuwa anayaongea Uncle Diamond. Yalikuwa yanatupa moyo, akasema tukaze moyo tusiangalie nyuma hata  hama watu wataongea,” anasema.

Magreth ni mwanafunzi wa kidato cha  tatu sasa na umri wa miaka 16.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *