
Dar es Salaam. Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo imeiomba Serikali itakayoingia madarakani kuendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya biashara, ili kuendelea kulipa soko hilo hadhi yake kama kitovu cha biashara kinachohudumia Tanzania na nchi jirani.
Kauli hiyo imetolewa leo, Oktoba 18, 2025, wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho yaliyofanywa na Serikali ya sasa, ambayo wamesema yameanza kuwapa amani na kuwajengea matumaini mapya katika shughuli zao za kila siku.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Renatus Mlelwa, amesema hatua mbalimbali zilizochukuliwa zimeongeza imani kwao kama wafanyabiashara, na kuwapa uhakika wa kuendeleza shughuli zao za kila siku kwa matumaini makubwa.
Amesema licha ya yaliyofanyika, pia alitaka maboresho zaidi katika mazingira ya biashara ikiwemo kuhakikisha soko la machinga lililopangwa kujengwa eneo la Jangwani linakamilika ili waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Mlelwa amesema utekelezaji wa mpango huo utaondoa mgongano uliopo kati ya wamiliki wa maduka na machinga, sambamba na kuboresha mwonekano wa Soko la Kariakoo ili liendane na hadhi yake ya kimataifa.
“Soko la Kariakoo litazamwe upya liwe na mazingira mazuri, kwani limebeba fursa nyingi katika ukanda huu. Machinga ni kimbilio la wengi wanaokwepa kodi inaleta uwiano usiokuwa sawa kwani kuwa wafanyabiashara wanajificha huko,” amesema Mlelwa.
Mlelwa pia alitaka Serikali ijayo kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa sheria inayowataka wageni kutokufanya shughuli za uchuuzi wa bidhaa ndogo ndogo ili kutoa fursa kwa wazawa kunufaika na fursa zilizopo.
“Wageni wabaki kama wawekezaji, wajenge viwanda, wazalishe bidhaa sisi tukanunue kutoka kwao tuje kuuza sokoni,” amesema.
Akizungumzia mazingira ya ufanyaji wa biashara kwa sasa sokoni hapo, Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mfaume Mfaume amesema wafanyabiashara wana amani tofauti na miaka michache nyuma, kwani sasa mambo mengi yanafanyika kwa maridhiano na kusikilizana.
Hiyo ni baada ya kufanyika kwa maboresho ya kodi kupitia Tume iliyoundwa huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiondoa kamata kamata iliyokuwa ikifanyika awali na kuanza kutumia maridhiano.
“Pia, marekebishi ya Sheria ya kodi yaliyofanyika sasa yameweka urahisi kwa wafanyabiashara kwani mtu mwenye mauzo ya Sh500 milioni halazimiki kutengeneza hesabu kwa kumlipa mhasibu anayetambuliwa bali unaweza kufanya hesabu mwenye ili uweze kulipa kodi,” amesema.
Pia, kuanzishwa kwa kodi elekezi ya forodha katika baadhi ya bidhaa ikiwemo vitenge imesidia kuondoa malalamiko yaliyokuwapo awali kwa wafanyabiashara hasa walipokuwa wakikadiriwa kodi kubwa kuliko bei watakayoitumia kuuza bidhaa sokoni.
Januari 25, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali iko mbioni kuanza ujenzi wa soko jipya eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam ikiwa sehemu ya mkakati wa kuwa na masoko katikati ya mji yatakayofanya kazi saa 24.