
Mbunge mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon Hizbullah amesisitiza kuwa, vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon vingali vinaendelea kwa malengo maalumu na kwa sura tofauti.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Manar, Hassan Fadhlullah, ambaye ni mbunge wa mrengo wa Uaminifu kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon amesema, katika vita vya hivi karibuni dhidi ya Lebanon, adui alikusudia kuviteka vijiji na miji ya kusini, akadhamiria kwa uchache kuikalia Litani ya kusini, kuwahamisha watu wake, kulidhibiti eneo hilo na kuanzisha makazi ndani yake, lakini istiqama ya Muqawama ilifelisha njama hiyo ya Israel na kuzuia kusini mwa Lebanon kughusubiwa na kukaliwa kwa mabavu.
Ameongeza kuwa, mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya raia na miundombinu ya Lebanon yanafanywa kwa lengo la kuwashinikiza watu wake hususan wa kusini mwa nchi hiyo wahame kwa nguvu na kusalimu amri.
Hassan Fadhlullah amesisitiza kuwa, vita vya mtawalia vingali vinaendelea dhidi ya eneo la kusini na watu wake, lengo likiwa ni kuzuia kujengwa upya eneo hilo na watu kuweza kurejea makwao; lakini vita hivyo vitapambanwa kwa uthabiti na kwa nguvu zote.
Mbunge huyo wa Hizbullah ameongezea kwa kusema: “hatuwezi kukubali sera potovu za ndani zinazokinzana na sheria na katiba. Kuna wanaokiuka sheria waziwazi kuridhia mashinikizo kutoka nje.”
Aidha, ametoa indhari kwamba mashinikizo yanayotolewa yatasababisha mripuko wa ndani na akatoa wito wa kuepuka kuitumbukiza nchi kwenye lindi la mkwamo.
Fadhlullah amekumbusha pia kuwa, Lebanon inakabiliwa na changamoto mbili za kimsingi: mashambulizi ya Israel na wajibu wa serikali wa kukabiliana na mashambulizi hayo; na vilevile suala la ujenzi upya wa maeneo yaliyoharibiwa na mashambulio ya Israel.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa serikali kubeba majukumu yake na kuzilazimisha pande zinazosimamia makubaliano zihakikishe mashambulio hayo yanakomeshwa. Ameeleza kuwa Muqawama utapokea hatua zozote chanya zinazochukuliwa na serikali, kwa sababu lengo ni kuhitimisha umwagaji damu na kukomesha uharibifu unaofanywa na Israel…/