Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imekataa ombi la utawala wa kizayuni wa Israel la kukata rufaa dhidi ya hati za kukamatwa waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita wa utawala huo ghasibu Yoav Gallant kuhusiana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi la kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.

Taarifa ya uamuzi uliotolewa na ICC imesema, ombi la Israel la kutaka kukata rufaa dhidi ya hati za kutiwa nguvuni Netanyahu na Gallant kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Ghaza halikubaliki kwa sababu hilo “si suala linaloweza kukatiwa rufaa.”

Katika uamuzi uliovuta hisia duniani kote, mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitangaza kwamba kuna “misingi ya kutosha” kuamini kuwa Netanyahu na Gallant wanabeba “jukumu la jinai” kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa huko Ghaza.

Hati za kukamatwa viongozi hao wawili wa kizayuni zilikabiliwa na hasira kali za Israel na Marekani, ambayo baadaye ilichukua hatua ya kuwawekea vikwazo maafisa waandamizi wa ICC.

Netanyahu alilaani hukumu hiyo akidai eti ni “uamuzi wa chuki dhidi ya Wayahudi,” huku Rais wa Marekani wa wakati huo Joe Biden akiuita “wa kushangaza.”

Mnamo mwezi Mei mwaka huu, utawala wa kizayuni uliiomba mahakama ya ICC ifute hati hizo huku ikifuatilia changamoto tofauti kuhusu iwapo ICC ina mamlaka ya kuendesha kesi hiyo.

Hata hivyo, mnamo Julai 16 Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilikataa ombi hilo ikisema, hakukuwa na “msingi wa kisheria” wa kufuta hati hizo wakati suala la mamlaka lingali linaendelea kushughulikiwa.

Wiki moja baadaye, Israel iliomba ruhusa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Julai, lakini siku ya Ijumaa majaji walilikataa ombi hilo, wakisema kuwa “suala hilo, kama lilivyowasilishwa na Israel, si suala linaloweza kukatiwa rufaa.”

“Kwa hivyo Mahakama inakataa ombi hilo,” ikaeleza ICC katika uamuzi wake wenye kurasa 13…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *