Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baghaei amelaani ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel, likiwemo shambulio la hivi karibuni dhidi ya gari lililokuwa limebeba familia ya Kipalestina wakati ikirejea kwenye makazi yao.

Akiashiria historia ya utawala wa Kizayuni ya kukiuka ahadi zake na mapatano ya usitishaji vita katika kadhia zinazofanana na hizo, Baghaei amebainisha wajibu wa moja kwa moja wa nchi zilizotoa dhamana katika suala hili, na akataka hatua madhubuti za jamii ya kimataifa zichukuliwe.

Amesema dunia inapasa kuchukua hatua madhubuti za kuulazimisha utawala wa Kizayuni kukomesha jinai zake, kuwaondoa askari wake vamizi kutoka Gaza, kuwapa watu wa Gaza utaratibu mzuri wa kupata chakula na misaada mingine ya dharura.

Baghaei amelaani vikali shambulio la hivi karibuni la Wazayuni huko Gaza, ambalo lilipelekea kuuawa shahidi watu 11 wakiwemo watoto 7 na wanawake 2. Aidha amekosoa hatua ya utawala huo ghasibu ya kukataa kutekeleza ahadi yake ya kufungua kivuko cha Rafah.

Mapema mwezi huu, utawala wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas zilikubaliana kutekeleza awamu ya kwanza ya mpango ya kusitisha vita Gaza; mpango ambao unatarajiwa kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari vya zaidi ya miaka miwili yaliyoanzishwa na Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 

Hata hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kukiuka makubaliano hayo kwa kutumia visizingizio mbali mbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *