
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uswidi amesisitiza kwamba Troika ya Ulaya imetokomeza uwezo wake wa kuwa na nafasi huru katika eneo la Asia Magharibi kwa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.
Jan Eliasson, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uswidi, ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, akiitaja hatua ya Troika ya Ulaya ya kuanzisha utaratibu wa “snapback” kuwa ni kurudi nyuma katika njia ya diplomasia na Iran.
Eliasson ameongeza kuwa, kurejeshwa vikwazo hivyo ni hatua nyingine ya kurudi nyuma kwa diplomasia yenye ufanisi kuhusiana na Iran.
Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Troika ya Ulaya ilidhuru nafasi yake huru katika eneo la Asia Magharibi kwa kupendekeza utaratibu wa “snapback” katika Baraza la Usalama, baada ya Marekani na utawala wa Israel kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.
Utaratibu huu unaziruhusu nchi wanachama katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA (Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani) kuanzisha mchakato wa kurejesha vikwazo vya awali vya Baraza la Usalama ikiwa Iran itakiuka majukumu yake ya JCPOA.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inautambua “utaratibu wa snapback” kuwa ni batili kisheria na kisiasa. Iran inaamini kuwa Marekani si mshirika tena katika mapatano ya JCPOA baada ya kujitoa rasmi katika mapatano hayo mwaka 2018 na hivyo haina haki ya kutumia mifumo iliyomo ndani ya mapatano hayo, ikiwa ni pamoja na snapback.
Iran inatumia hoja kwamba, nchi za Ulaya pia hazijatekeleza wajibu wao chini ya mapatano ya JCPOA, hivyo haziwezi kuituhumu Iran kuwa imekiuka makubaliano hayo na kuanzisha utaratibu wa snapback. Iran na baadhi ya nchi, kama vile Russia na Uchina, zinaamini kwamba, kuanzisha utaratibu wa snapback kunahitaji maafikiano au mchakato mahususi wa kisheria ambao haujafuatwa katika matukio ya hivi majuzi.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, nchi ambayo imejiondoa katika makubaliano haiwezi tena kutumia taratibu zake. Kwa hivyo, jaribio la Marekani la kuwezesha utaratibu wa snapback katika miaka inayofuata halina uhalali wa kisheria na ni kinyume na vipengee vya azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.