Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa umoja huo ulioanzishwa miaka 80 iliyopita unaweza kufilisika ikiwa nchi wanachama hazitolipa michango yao kwa ukamilifu.

Antonio Guterres ametoa indhari hiyo wakati akiwasilisha bajeti ya kawaida ya taasisi hiyo kuu kimataifa ya mwaka 2026 ya dola bilioni 3.238.

Kiwango hicho kilichofanyiwa marekebisho ni pungufu kubwa kutoka dola bilioni 3.715 zilizokuwa zimeombwa awali na ni pungufu kwa asilimia 15.1 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu wa 2025.

Bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa hufadhiliwa kupitia michango ya lazima kutoka nchi wanachama, michango ambayo hulingana na tathmini ya uwezo wa kila nchi na hujikita kwa programu za msingi na operesheni za Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Katibu Mkuu.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yenye wajibu wa kushughulikia fedha na masuala ya utawala ya UN, Guterres ameelezea taswira tete iliyopo na kwamba kucheleweshwa kwa michango kunatishia kufuta uwezo wa kifedha wa shirika hilo kuu kimataifa na kukwamisha operesheni muhimu.

Katibu Mkuu ameonya kwamba, hali ya sasa ya ukata itakuwa na madhara makubwa mwakani na hadi 2027.  Kiwango kikubwa cha malimbikizo ya michango mwishoni mwa mwaka jana yakiwa ni jumla ya dola milioni 760, yakigubikwa na marejesho ya lazima ya dola milioni 300 kwa nchi wanachama kuanzia mwaka 2026, kinaondoa takribani asilimia 10 ya fedha za bajeti zilizoko sasa.

“Kucheleweshwa kokote kwa makusanyo ya fedha mwanzoni mwa mwaka, hutulazimu kupunguza matumizi yetu zaidi… na kisha tutalazimika kurejesha dola milioni 600 mwaka 2027, au sawa na asilimia 20 ya bajeti,” amesema Guterres.

“Hii ina maana mbio za kuelekea kufilisika,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza udharura wa kupunguza malimbikizo na kusitisha utaratibu wa kurejesha kwa nchi wanachama fedha za bajeti ambazo hazijatumika…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *