Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeliengua katika mchakato wa kuwania Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), jina la Mwenyekiti wa Mtibwa Sugar, Said Suud.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF leo, imeeleza kuwa Suud ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo, ameenguliwa kwa kukosa sifa kwa mujibu wa kanuni ya 9:7 na 10:3.

Kuenguliwa kwa Suud kunafanya kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa TPLB kubaki kwa Nassor Idrissa na Hoseah Lugano.

Idrissa ni Rais wa Azam FC huku Lugano akiwa Mwenyekiti wa Namungo FC.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa TPLB imebaki na mgombea mmoja ambaye ni Hassan Muhsin huku Kheri Missinga akienguliwa.

Missinga ambaye ni mwenyekiti wa KMC, ameondolewa kwenye mchakato kwa vile hakutokea katika zoezi la usaili, Oktoba 15, 2025.

Majina mawili yamepitishwa kuwania nafasi ya Mjumbe wa kuwakilisha Klabu za Ligi Kuu ambayo ni Japhet Makau na Gilbert Nkoronko.

Hillary Ndumbaro na Waziri Gao wamepitishwa kuwania nafasi ya Ujumbe wa Kuwakilisha Klabu za Championship.

Wakati huohuo, Azimkhan Akber amepitishwa kuwania ujumbe wa kuwakilisha Klabu za First League.

Uchaguzi Mkuu wa TPLB umepangwa kufanyika Novemba 29, 2025 hapa Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *