Liverpool, England. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool watashuka dimbani leo kuvaana na Mashetani Wekundu, Manchester United katika mechi ya ligi itayopigwa kwenye Uwanja wa Anfield.

Rekodi zinaonyesha kuwa mara ya mwisho United kuchomoza na ushindi kwenye Uwanja wa Anfield ilikuwa Januari 2006 ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Wayne Rooney.

Manchester United haijawahi kushinda tena Anfield katika michezo tisa mfululizo ya Ligi Kuu wakati Liverpool imeshinda michezo saba na kutoka sare sita dhidi ya wapinzani wao hao wa jadi.

Hata hivyo, Klabu hiyo inayonorewa na kocha, Ruben Amorim imekuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo kwenye mechi za ugenini kwani haijashinda katika mechi zake nane za ugenini za Ligi Kuu ikitoa sare mara mbili na kupoteza mara sita.

Mara ya mwisho United kushinda ugenini ilikuwa Januari mwaka huu, ilipoilaza Fulham bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu.

Kwa sasa Liverpool inapitia kipindi kigumu ikiwa imepoteza michezo mitatu mfululizo katika mashindano yote, hali ambayo haijawahi kumtokea kocha Arne Slot.

Hata hivyo, Majogoo hao wa Anfield wamekuwa na rekodi nzuri katika Uwanja wao wanyumbani kwani wakiwa Anfield, Liverpool wameshinda michezo yote mitano ya msimu huu katika mashindano yote.

Kwa upande mwingine, United wanakutana na Liverpool waliojeruhiwa ugenini lakini pia, wanakutana na Liverpool wenye rekodi ya kutisha kwenye Uwanja wa nyumbani.

Nyota wa Misri Mohamed Salah ndiye mchezaji mwenye mchango mkubwa zaidi wa mabao dhidi ya Manchester United katika historia ya Ligi Kuu England akiwa amehusika kwenye mabao 19  akifunga 13 na kutoa pasi sita za mabao.

Ikiwa United watashinda, Amorim atakuwa kocha wa tatu katika historia ya EPL kushinda mechi mbili dhidi ya mabingwa watetezi akiwa ugenini wengine waliowahi kufanya hivyo ni Manuel Pellegrini na Antonio Conte.

Hali za majeruhi

Liverpool bado watamkosa Alisson Becker, lakini Ryan Gravenberch anaweza kurejea uwanjani huku Ibrahima Konaté akitarajiwa kurejea mazoezini kabla ya mechi.

Kwa upande wa United, hali ni shwari zaidi Noussair Mazraoui na Lisandro Martínez pekee ndio wanaotarajiwa kukosekana kwenye mchezo wa leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *