f

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Reza Sepehri
    • Nafasi, BBC

Katika kipindi cha nusu karne iliyopita, baadhi ya mali na majengo yanayomilikiwa na serikali ya Iran au taasisi zake tanzu nje ya nchi, hususan katika nchi za Magharibi, zimekuwa kitovu cha migogoro ya kisheria, kisiasa na kiusalama.

Migogoro hii inajumuisha; kuzishikilia, kunyang’anya, uhamisho wa lazima wa umiliki au usimamizi, kufungwa kwa vituo vya kidini na kitamaduni, pamoja na madai ya kifedha yanayotokana na vikwazo.

Katika mengi ya matukio haya, suala sio tu umiliki wa jengo, lakini pia mgongano wa mifumo ya kisheria na kisiasa, kanuni za kinga ya kidiplomasia katika Mkataba wa Vienna, mstari kati ya mali rasmi ya serikali na ya kibiashara, kanuni za kupambana na ugaidi, na mbinu ya kutekeleza hukumu dhidi ya mali ya kigeni – yote haya yanahusika katika kuamua hatima ya mali hizi.

Utata huu umesababisha baadhi ya kesi hizi kuchukua miaka kusuluhishwa, na idadi kamili ya mali zisizohamishika za Iran nje ya nchi bado hazijulikani.

Katika ripoti hii, tumechunguza idadi ya majengo haya muhimu na kesi zao; kutoka New York hadi kwenye miji mingine ya nchi za Ulaya.

Pia unaweza kusoma

650 Fifth Avenue, New York

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Jengo lililoko mtaa wa 650 Fifth Avenue katikati mwa eneo la biashara la Manhattan ni moja ya mali ya thamani ya Iran nje ya nchi na kitovu cha mojawapo ya migogoro mirefu zaidi ya kisheria kati ya Iran na Marekani.

Jengo hilo la ghorofa 36 lilijengwa mwaka 1978, mwaka mmoja kabla ya Mapinduzi ya Iran, kwa ufadhili wa Wakfu wa Pahlavi, kwa ajili ya uwekezaji na kutoa misaada, na baada ya mapinduzi, lilibadilishwa jina na kuitwa “Alavi Foundation,” chini ya usimamizi wa Mostazafan Foundation.

Madhumuni yaliyotajwa ya jengo hilo yalikuwa kupata mapato endelevu kwa kukodisha ofisi ili kusaidia programu za kitamaduni na elimu za Iran nje ya nchi.

Baada ya mapinduzi hayo, Wakfu wa Alavi ulikuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ukibakisha asilimia 60 ya hisa, huku asilimia 40 nyingine zikiwa za ASA, mshirika wa Benki ya Kitaifa ya Iran.

Serikali ya Marekani ilidai mwaka 2008 kuwa muundo huo wa usimamizi ni kwa lengo la kukwepa vikwazo na Wakfu wa Alavi ulihamisha mamilioni ya dola kwenda Benki ya Kitaifa ya Iran kupitia ASA.

Mnamo mwaka 2017, mahakama ya shirikisho iliamua kulichukua jengo hilo. Lakini 2019, Mahakama ya Rufaa ya New York ilibatilisha uamuzi huo kwa sababu ya ukiukaji wa utaratibu na tathmini isiyofaa ya ushahidi, na kurudisha kesi hiyo kwa mahakama ya wilaya ili iangaliwe upya.

Kesi ya jengo bado inasubiri, na hatima yake ya mwisho haijulikani. Jengo hilo linakadiriwa kuwa na thamani kati ya dola milioni 500 hadi bilioni moja.

Ubalozi wa zamani wa Iran

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Ubalozi wa zamani wa Iran huko Washington, D.C., katika mtaa wa 3005 Massachusetts Avenue, ulijengwa mwaka 1959. Jengo hili, lenye eneo la takriban mita za mraba 3,400, kilikuwa kitovu cha shughuli za kidiplomasia za Iran wakati uhusiano na Marekani ulipoanzishwa wakati wa enzi ya Pahlavi.

Baada ya tangazo rasmi la kukata uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili Aprili 7, 1980, baada ya kutekwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran, wanadiplomasia wa Iran walifukuzwa nchini Marekani.

Tangu wakati huo, jengo hilo limefungwa rasmi na kutelekezwa. Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna, umiliki wake wa kisheria unabakia kwa serikali ya Iran, lakini serikali ya Marekani inawajibika kwa ulinzi na matengenezo, gharama za matengenezo hutokana na kodi za mali nyingine za Iran nchini Marekani.

Makazi ya balozi wa zamani, yaliyo karibu na jengo la ubalozi, ni jumba lenye vyumba zaidi ya 40 na eneo la takriban mita za mraba 1,600. Makazi hayo, pamoja na mali nyingine za kidiplomasia za Iran, yalikabidhiwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani 1980.

Jengo hilo liliripotiwa kufanyiwa ukarabati katika miaka ya 1990 na kukodishwa mwaka 1995, lakini baadaye liliachwa kukodishwa kutokana na madeni ya mpangaji.

Mali za Iran nchini Marekani

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Mbali na jengo la ubalozi na makazi ya balozi mjini Washington, serikali ya Marekani inashikilia zaidi ya mali nyingine 10 zinazomilikiwa na Iran chini ya usimamizi wa Ofisi ya Balozi za Kigeni tangu 1980. Mali hizi ni pamoja na makazi ya kidiplomasia, nyumba za kibalozi na makazi katika miji kama vile New York, Chicago, Houston, na San Francisco.

Huko New York, nyumba kwenye mtaa wa East 69th Street ilikodishwa mwaka 2002 na iliripotiwa kuleta takriban dola za kimarekani 500,000 kwa mwaka.

Huko Chicago, majengo mawili ya zamani ya ubalozi yameunganishwa kuwa jengo moja na kukodishwa. Huko San Francisco, jengo la zamani la ubalozi wa Iran lenye vyumba 17 kwenye Mtaa wa Washington liliripotiwa 2019 kugharimu dola milioni 5 kukarabati.

Kulingana na ripoti rasmi iliyochapishwa mwaka 2010, jumla ya mapato ya kukodisha kutokana na majengo haya kutoka 1990 hadi 2008 ni karibu dola milioni 10, lakini gharama za matengenezo katika kipindi hicho ni kubwa zaidi.

Kampuni ya Mafuta

dc

Kesi hiyo ya Crescent inatokana na mkataba wa miaka 25 wa mauzo ya gesi uliotiwa saini mwaka 2001 kati ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran (NIOC) na Crescent Petroleum ya Falme za Kiarabu.

Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran ililazimika kusambaza gesi ya futi za ujazo milioni 500 kwa siku, lakini kulingana na hati za kisheria, haikufanya usambazaji huo tangu 2005 na kusitisha mkataba 2010.

Crescent ilifungua kesi, na jopo la usuluhishi la kimataifa 2021 liliamuru Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran kulipa hasara ya dola bilioni 2.43.

Iran ilikataa uamuzi huo, na Crescent ilianza kutwaa mali ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran kote ulimwenguni kupitia hatua za kisheria.

Moja ya majengo hayo ni “Jengo la Kampuni ya Mafuta ya Iran” huko London, ambalo kwa takriban nusu karne lilikuwa ishara ya uwepo wa kiuchumi wa Iran katika mji mkuu wa Uingereza.

Jengo hilo la kifahari, lenye thamani ya takriban pauni milioni 100, liko katika karibu na Bunge la Uingereza. Jengo hilo limekuwa makao ya matawi ya wizara ya mafuta ya Iran barani Ulaya tangu miaka ya 1970, lakini sasa ni mojawapo ya mali muhimu zaidi za Iran zilizotwaliwa nje ya nchi kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Crescent.

Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran ilijaribu kubadilisha umiliki wa jengo, lakini Aprili 2024, mahakama ya London iliamua kwamba uhamishaji wa umiliki ni kwa lengo la kuficha mali.

Iran ilikata rufaa, lakini Mahakama ya Rufaa ya Uingereza hatimaye ilikubali uamuzi huo, na hivyo kufungua njia kwa jengo hilo kuuzwa au kupewa Crescent. Uamuzi huu unachukuliwa kuwa moja ya matokeo mabaya zaidi ya mahakama kwa Iran.

Na huko Rotterdam, Uholanzi, kutaifishwa kwa ofisi ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Irani (NIOC) kulianza Mei 2022. Jengo hilo liliuzwa kwa mnada wa umma kwa kampuni ya Uholanzi ya Hovel Fasthood BV.

Januari 2025, Mahakama ya Wilaya ya Rotterdam ilitangaza uhamishaji wa umiliki, ikikataa pingamizi la NIOC. Uamuzi huu ulimaliza uwepo wa NIOC nchini Uholanzi na kuweka njia kwa hatua kama hizo katika nchi zingine.

Crescent pia inaendelea kuchukua hatua za kisheria katika nchi nyingine, kama vile Ugiriki na UAE, ili kupata mali ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Iran.

Mali za Iran huko Canada

Kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Haki kwa Wahanga wa Ugaidi mwaka 2012, serikali ya Canada iliitaja Iran kama “serikali inayofadhili ugaidi” na kuruhusu hukumu za mahakama za Marekani dhidi ya Iran zitekelezwe katika ardhi ya Canada.

Sheria hiyo inaruhusu waathiriwa wa mashambulizi yanayohusishwa na makundi kama vile Hezbollah ya Lebanon na Hamas, kulenga mali zisizo za kidiplomasia za serikali ya Iran kwa ajili ya kulipwa fidia.

Mwaka 2016, Mahakama ya Juu ya Ontario, ikitoa mfano wa sheria hiyo hiyo, iliamuru kukamatwa na kuuzwa kwa mali mbili zinazohusiana na serikali ya Iran: Kituo cha Utamaduni cha zamani cha Iran huko Ottawa na Kituo cha Mafunzo ya Iran huko Toronto.

Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, ingawa mali hizo zilisajiliwa kwa majina ya taasisi za kitamaduni, kwa hakika zilikuwa “zinazomilikiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Mali hizo hatimaye ziliuzwa: mali ya Ottawa kwa Canada dola milioni $ 26.5 na mali ya Toronto kwa Canada dola milioni 1.85 milioni. Mahakama iliamuru fedha zigawiwe miongoni mwa familia za wahanga wa mashambulizi yaliyohusishwa na Iran, ikiwa ni pamoja na shambulio la bomu la mwaka 1983 katika makao makuu ya Jeshi la Wanamaji la Marekani huko Beirut.

Uamuzi wa mahakama pia ulibainisha kuwa mali ya Ottawa ilikuwa na uhusiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Serikali ya Iran ilikata rufaa ikiita uamuzi huo ni “ukiukwaji wa kinga ya serikali na kanuni za sheria za kimataifa,” lakini Mahakama Kuu ya Canada ilikataa rufaa ya Iran mwaka 2018.

Kwa hiyo, uuzaji na uhamisho wa mapato ulikamilika, na kesi hiyo ikawa ya kwanza ya mafanikio ya utekelezaji wa Sheria ya Haki kwa Waathiriwa wa Ugaidi dhidi ya mali ya Iran nchini Canada.

Vituo vya Kiislamu katika Ulaya

DFC

Chanzo cha picha, Abna24

Kituo cha Kiislamu cha Uingereza ni taasisi ya Kishia ambayo imekuwa ikifanya kazi London tangu mwaka 1995. Ukosoaji dhidi ya kituo hicho, ulipata nguvu baada ya ibada mbili za kumbukumbu ya Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha IRGC, kufanywa 2020.

Kufuatia haya, Kamisheni ya Waqfu ya Uingereza na Wales ilianzisha uchunguzi rasmi juu ya utawala wa kituo hicho, uwazi wa kifedha na matakwa ya kisheria.

Jengo la kituo hicho lilifungwa kwa muda Julai 2023. Tume ilieleza kuwa sababu ya kufungwa ni ukosefu wa bima halali, na kituo kilifunguliwa baada ya kupatikana kwa bima. Uchunguzi wa unaendelea, na tume imewataka wasimamizi kuweka wazi kuhusu ufadhili, uteuzi wa msemaji na maudhui yanayochapishwa.

Kituo cha Kiislamu Hamburg

FGV

Chanzo cha picha, Getty Images

Kituo cha Kiislamu cha Hamburg, mojawapo ya vituo vikongwe vya Kiislamu vya Kishia barani Ulaya, kilianzishwa katika miaka ya 1950 na wahamiaji wa Iran na kupanuliwa katika miaka ya 1960 kwa kufunguliwa Msikiti wa Imam Ali.

Julai 2024, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ilipiga marufuku Kituo cha Kiislamu cha Hamburg na taasisi kadhaa tanzu, ikitangaza kwamba kituo hicho ni “chombo cha kukuza itikadi kali ya Kiislamu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran” nchini Ujerumani na “kinaongozwa moja kwa moja na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Iran.”

Wakati huo huo, Polisi ya Shirikisho walikagua majengo 53 yanayohusiana na kituo hicho katika majimbo manane na kuzuia mali zao. Serikali ya Ujerumani ilisema hatua hiyo inalenga kulinda demokrasia. Iran ililaani uamuzi huo kama kitendo cha uadui ambacho kinakiuka kanuni za haki za binadamu.

Msikiti wa Imam Ali ulioko Copenhagen pia ni kituo kikubwa zaidi cha Washia nchini Denmark, ambacho kimekuwa katika vichwa vya habari katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ripoti za ufadhili kutoka taasisi za Iran, imamu wa msikiti huo ana uhusiano na ubalozi wa Iran, anafuatiliwa na idara ya usalama ya Denmark.

Ofisi ya Iran Air

v

Chanzo cha picha, Getty Images

Ofisi ya Iran Air katika mtaa wa 63 Champs-Elysees mjini Paris ilikuwa mojawapo ya majengo ya kibiashara ya Iran yanayotambulika zaidi barani Ulaya.

Ofisi hii iliyopo katika maeneo ya bei ghali jijini Paris, imeingia kwenye vichwa vya habari miaka ya hivi karibuni kutokana na mzozo wa kisheria kati ya mmiliki wa jengo hilo Mfaransa na Iran Air.

Kampuni inayomiliki inadai Iran Air haijalipa kodi ya jengo hilo kwa miaka kadhaa. Iran Air inasema vikwazo vya benki vya Marekani vimezuia fedha kuhamishwa kutoka Iran hadi kwenye akaunti zake za benki nchini Ufaransa.

Kesi inayohusiana na jengo hili imekuwa ikiendelea katika mahakama ya Paris tangu Februari 2019, na IranAir inasema inafuatilia hatua za kisheria kupitia mawakili wake ili kuzuia ofisi hiyo kuhamishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *