Mwili wa Odinga umezikwa Jumapili jioni kwenye makaburi ya familia huko Kang’o Ka Jaramogi, Bondo na kuhudhuriwa na watu wachache wa familia. Wanajeshi wa Kenya walifyatua mizinga 17 kama ishara ya heshima kwa mwendazake.
Kabla ya hapo hafla kubwa ya mazishi ya aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya ilifanyika Jooust Bondo huku kukiwa na ulinzi mkali kufuatia vurugu mbaya zilizotokea katika mji mkuu wa nchi hiyo wakati wa ibada ya kitaifa.
Maelfu ya Wakenya na watu mashuhuri kutoka kote barani Afrika wamehudhuria mazishi hayo ya Raila. Waombolezaji walishindwa kujizuia wakati msafara wa wanajeshi uliokuwa umebeba jeneza ulipokuwa ukiingia katika ukumbi huo muda mfupi baada ya saa 9.20 asubuhi.
Hafla ya ibada hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi kadhaa nchini Kenya na Afrika. Mjane wa Odinga, Ida Odinga aliwashukuru Wakenya, majirani wa eneo hilo, na jumuiya ya kimataifa kwa kuungana na familia kumuomboleza kiongozi huyo mashuhuri wa kisiasa.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi, gavana wa jimbo la Siaya James Orengo alisema Raila alifurahia amani na maridhiano katika maisha yake yote ya kisiasa.
“Sisi ni mayatima”
Mwili wa Odinga, ulisafirishwa hadi kwao Bondo karibu na kaunti ya Siaya. Kabla ya kufikishwa Bondo, mwili wa Odinga uliagwa na umati mkubwa wa waombolezaji uliojitokeza katika mji wa magharibi mwa Kenya, Kisumu. Watu kadhaa walijeruhiwa wakati wa maombolezo ya Kisumu.
Vilio vya “Baba” na “Sisi ni mayatima” vimesikika miongoni mwa maelfu ya watu waliomiminika mitaani mjini Kisumu, ngome kuu ya uungwaji mkono wa Odinga, wakati jeneza lake lilipowasili kwa helikopta katika uwanja wa jiji hilo.
Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 80, alifariki Jumatano nchini India kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa mshtuko wa moyo, na kusababisha majonzi makubwa kote nchini, hasa katika eneo la magharibi mwa Kenya ambako kabila lake la Wajaluo linatawala.
Waombolezaji walivunja vizuizi vya usalama na kupanda kuta za uwanja na majengo jirani ili kuweza kuona jeneza. Wasaidizi wa dharura walisema waliwatoa zaidi ya watu 100 walioumia kutoka uwanjani.
“Bila Baba, tumekufa. Hatuna pa kwenda,” alisema Don Pelido, mwenye umri wa miaka 20, aliyekuwa amebanwa dhidi ya kizuizi kimoja.
Mhandisi wa siasa za Kenya
Wengi walihofia kuwa shughuli ya Jumamosi ingesababisha maafa, ikizingatiwa vurugu zilizotokea kwenye kumbukumbu zilizofanyika Nairobi wiki hii.
Alhamisi, vikosi vya usalama vilifyatua risasi kutawanya umati uliokuwa ukisonga mbele katika uwanja wa Nairobi ambako Odinga alikuwa amewekwa kwa heshima za mwisho, na kuua angalau watu watatu. Ijumaa, katika maombi ya kitaifa yaliyoongozwa na Rais William Ruto katika uwanja mwingine, msongamano wa waombolezaji uliwaua angalau watu wawili na kujeruhi kadhaa.
Kwa hakika, Odinga alikuwa kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi wa kizazi chake nchini Kenya. Alihudumu kama Waziri Mkuu kati ya 2008 na 2013, ingawa hakuwahi kufanikiwa kushinda urais licha ya kujaribu mara tano.
Hata hivyo, aliwashinda wapinzani wengi na anasifiwa kama mhusika mkuu katika kurejesha demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya miaka ya 1990, na kusimamia katiba ya mwaka 2010 iliyosifiwa sana.
Kifo chake kimeacha pengo la uongozi katika upinzani, huku wakosoaji wakimlaumu kwa kushindwa kuandaa mrithi.