KIPIGO cha bao 1-0 ilichopokea Yanga juzi Jumamosi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili, ilihitimisha simu 315 sawa na miezi 10 na siku 11 kwa kikosi hicho kuruhusu maumivu hayo tena.

Kabla ya mechi hiyo, Yanga ilishuka dimbani mara 37 bila ya kupoteza ‘unbeaten’ katika mashindano yote. Mara ya mwisho ilipoteza Desemba 7, 2024 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipofungwa mabao 2-0 na MC Alger ikiwa ugenini. Kisha ikapoteza tena Oktoba 18, 2025 ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers, mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi hizo 37, zilikuwamo sita za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni; TP Mazembe 1-1 Yanga, Yanga 3-1 TP Mazembe, Al Hilal 0-1 Yanga, Yanga 0-0 MC Alger, Wiliete 0-3 Yanga na Yanga 2-0 Wiliete.

Ligi Kuu Bara zipo 21 ambazo ni; Yanga 3-2 Mashujaa, Yanga 4-0 Tanzania Prisons, Dodoma Jiji 0-4 Yanga, Yanga 5-0 Fountain Gate, Yanga 4-0 Kagera Sugar, Yanga 6-1 KenGold, JKT Tanzania 0-0 Yanga, KMC 1-6 Yanga, Yanga 2-1 Singida BS, Mashujaa 0-5 Yanga, Pamba Jiji 0-3 Yanga, Tabora United 0-3 Yanga, Yanga 1-0 Coastal Union, Azam 1-2 Yanga, Fountain Gate 0-4 Yanga, Yanga 3-0 Namungo, Tanzania Prisons 0-5 Yanga, Yanga 5-0 Dodoma Jiji, Yanga 2-0 Simba, Yanga 3-0 Pamba Jiji na Mbeya City 0-0 Yanga.

Ngao ya Jamii ni mechi moja tu; Yanga 1-0 Simba, lakini kwa upande wa Kombe la FA zilikuwa mechi sita, hali ilikuwa hivi; Yanga 5-0 Copco, Yanga 3-1 Coastal Union, Yanga 2-0 Songea United, Yanga 8-1 Stand United, Yanga 2-0 JKT Tanzania na Yanga 2-0 Singida Black Stars.

Pia kwenye Kombe la Muungano, Yanga ilicheza mechi tatu, iliifunga KVZ mabao 2-0, ikaichapa Zimamoto kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya 1-1, kisha fainali ikaichapa JKU 1-0.

YANG 01

MWANZO MPYA
Yanga haina budi kupindua matokeo ya kupoteza ugenini mbele ya Silver Strikers ili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers juzi Jumamosi, kimefanya ajira ya Kocha Romain Folz kufikia tamati ndani ya Yanga. Katika mechi ya marudiano Oktoba 25, 2025 jijini Dar, Yanga inalazimika kushinda kwa tofauti ya mabao angalau 2-0 ili kufuzu makundi.

Katika mechi ya juzi ikiwa ni ya kwanza kwenye hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Bingu jijini Lilongwe, Malawi, bao pekee lilifungwa dakika ya 76 na mshambuliaji, Andrew Joseph, akiunganisha pasi ya Ernest Petro.

YANGA ILIAMKA MAPEMA, LAKINI…
Yanga ilianza kwa kasi ikitawala eneo la kati ikijaribu kuisumbua safu ya ulinzi ya Silver Strikers.
Hata hivyo, safu ya ulinzi ya wenyeji ikiongozwa na Nickson Mwase na Maxwell Paipi ilikuwa ngumu na kuzima mashambulizi yote ya Yanga.

Dakika ya 28, Silver Strikers ilikaribia kufunga kupitia Stanie Davie, lakini shuti lake liliishia mikononi mwa kipa wa Yanga. Kipindi cha kwanza kilimalizika bila kufungana, huku timu zote zikirudi mapumzikoni zikisaka mbinu mpya.

Andy Boyeli aliyekuwa mshambuliaji kiongozi wa Yanga, alipoteza nafasi na kuikosesha timu hiyo uwezekano wa kwenda mapumziko ikiwa mbele. Hata hivyo, dakika 45 za kwanza hakukuwa na mbabe.

YANG 02

WALIPOPATIA WENYEJI
Kocha wa Silver Strikers, Etson Kadenge Mwafulirwa, alifanya mabadiliko muhimu kwa kumtoa Zebron Kalima na kumuingiza Ernest Petro, mabadiliko yaliyogeuza kabisa sura ya mechi.

Petro aliongeza kasi na ubunifu katika eneo la kiungo, akawa kiungo wa mawasiliano kati ya safu ya kati na washambuliaji.

Dakika ya 76 alitoa pasi tamu iliyopenya katikati ya walinzi wa Yanga, ikamkuta Andrew Joseph ambaye aliitumia vizuri kuipa Silver Strikers ushindi huo muhimu.

YANG 04

MATATIZO YA YANGA
Yanga Ilijitahidi kurudi mchezoni ikitafuta bao la kusawazisha, lakini ilikosa umakini katika eneo la hatari. Mashuti kadhaa ya nyota wa Yanga akiwemo Pacôme Zouzoua hayakuwa na madhara, huku Silver Strikers ikilinda kwa nidhamu hadi kipyenga cha mwisho.

Eneo la kiungo, Yanga ilionekana kucheza karibu sana, jambo lililoruhusu Silver Strikers kuzuia mipira kwa urahisi katikati.

Viungo wa Silver Strikers, hasa Ernest Petro aliyeingia kipindi cha pili, walipata nafasi ya kupandisha timu kirahisi na kuiweka Yanga hatarini. Aziz Andabwile, Mohamed Doumbia na Mudathir Yahya pale katikati walionekana kushindwa kuonyesha makali.

Baada ya dakika ya 60, Yanga ilionekana kuchoka kimwili, jambo lililosababisha Silver Strikers kuanza kushambulia zaidi.

Hata hivyo, mwisho wa mechi Yanga ilionekana kutawala kwa takwimu nyingi ikiwemo umiliki wa mpira Umiliki wa mpira asilimia 54 kwa 46, pia ikipiga mashuti 11 dhidi ya 9. Kati ya hayo, matatu yalilenga lango, Silver Strikers ilikuwa na manne.

Kwa jumla, Yanga haikuwa na muunganiko mzuri, ukiangalia bao ililoruhusu utagundua hilo kwani pasi nne zilizopigwa kuanzia kwa kipa wa Silver Strikers, hadi nyavu zinakwenda kutikiswa, wachezaji walipitwa kama wamesimama.

Kipa George Chikooka baada ya kuukamata mpira, akaanzisha mwendo upande wake wa kulia kwa McDonald Lameck ambaye alimpasia kiungo wa kati Uchizi Vunga aliyeukokota mpira kwa muda mrefu hadi amekaribia boksi la Yanga, ndipo akamuachia Ernest Petro aliyempa pasi mfungaji Andrew Joseph na kumuacha kipa wa Yanga, Djigui Diarra na mabeki wake, Dickson Job na Ibrahim Bacca washindwe la kufanya.

YANG 03

NINI KIFANYIKE
Pengine kukosekana kwa nyota takribani 11 kwa wiki mbili kipindi cha maandalizi ya mechi hiyo, inaweza kuwa sababu ya Yanga kutokuwa vizuri.

Nyota hao walikuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa zilizokuwa zikicheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026. Pacome aliyeanza kikosini na Duke Abuya aliyeingia kipindi cha pili, walikuwa wa mwisho kuungana na wenzao nchini Malawi.

Nyota wengine waliosekana kwa muda mrefu ni Prince Dube, Celestine Ecua, Lassine Kouma, Offen Chikola, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Israel Mwenda. Aziz Andabwile na Dickson Job walirudi mapema klabuni wakitokea kikosi cha Taifa Stars kwani hawakenda Dubai kucheza na Iran.

Kati ya wale waliokosekana kwenye maandalizi kwa muda mrefu, Mwenda, Bacca na Pacome ndio pekee walioanza kikosini. Ecua, Dube na Abuya walikuja kuingia baadae. Uchovu unaweza kuwa sababu lakini Yanga haina budi kuimarisha eneo la katikati ya uwanja kuanzia kiungo na ulinzi. Silver Strikers ilikuwa ikifanya vizuri eneo hilo kupitia Uchizi Vunga.

KAULI YA KOCHA KADENGE
Kocha Kadenge hakuficha furaha yake baada ya mechi, lakini alionekana mwenye tahadhari kubwa akisema: “Nimefurahia ushindi huu, lakini kazi haijaisha. Tunakwenda Dar es Salaam kupambana tena. Njia bora ya kujilinda ni kushambulia, hivyo tutajiandaa vizuri.”

Kocha Romain Folz naye alitoa maoni yake baada ya mechi hiyo kabla ya kusitishiwa kibarua chake akisema: “Nafikiri tulikuwa wabaya katika kumalizia nafasi zetu, lakini tutaboresha hilo na kufanya vizuri Jumamosi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *