Sumbawanga. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imepanga kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji, mpango mkubwa utakaolenga kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha ustawi wa wananchi nchini.
Akihitimisha kampeni zake leo, Jumapili Oktoba 19, 2025, katika mkutano uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Kizwite, Sumbawanga mjini mkoani Rukwa, Samia amewataka wananchi wa mkoa huo kuichagua CCM katika ngazizote ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika miaka iliyopita.
Amesema miradi ya maji safi na salama kupitia mpango huo wa gridi ya taifa itamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji na hivyo kuboresha afya, uchumi na maisha ya Watanzania.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite Manispaa ya Sumbawanga kusikiliza sera za mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM
“Kama ulivyo mpango wa umeme, maji nayo yana umuhimu ule ule. Tukipata uhakika wa maji, kilimo cha umwagiliaji kitakuwa na tija kubwa na maisha ya watu yataboreka zaidi,” amesema Samia.
Amesema miradi ya maji ni miongoni mwa miradi ghali nchini, kwa sababu gharama zake mara nyingine hulingana na zile za ujenzi wa barabara, lakini Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo muhimu.
Amefafanua kuwa gridi hiyo ya taifa ya maji itatumia vyanzo vikubwa vitatu vya Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria.
“Tunazungumza kuyatoa maji Ziwa Tanganyika hadi huku, na pengine yaende mbali zaidi. Gridi hii itahusisha njia tatu zitakazounganika ili kuwa na hifadhi ya maji mengi. Endapo upande mmoja utakosa maji, gridi itagawa maji kwenda upande huo. Hii ndiyo dhamira yetu — kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama,” amesema Samia.
Kuhusu sekta ya kilimo, mgombea huyo amesema Serikali imetenga bajeti maalumu ya ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima, na kumtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo kusaidia wakulima.
“Tumetoa mbolea nyingi, wakulima wamezalisha kwa wingi. Sasa tunahitaji maghala ya kuhifadhi mazao na fedha za kununua mahindi yao. Tukiweza kuuza nje, tutapata nafasi ya kuhifadhi mengine na kuongeza kipato cha wakulima wetu,” amesema.

Kada mpya wa CCM, Ezekiel Wenje akizungumza wakati mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite Manispaa ya Sumbawanga
Samia ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuelekea katika mapinduzi ya kilimo cha umwagiliaji na ifikapo mwaka 2030, inalenga kuwa na angalau hekta milioni tano za kilimo cha umwagiliaji.
“Tukifika hatua hiyo, Tanzania itakuwa kinara wa uzalishaji wa chakula barani Afrika, na itaweza kulisha sehemu kubwa ya bara letu na kwingineko duniani,” amesema.
Kuhusu Mkoa wa Rukwa, Samia ameahidi endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza, Serikali itamalizia maboresho ya uwanja wa ndege wa Sumbawanga, sambamba na kukuza sekta ya utalii katika eneo hilo lenye vivutio vingi vya asili.
“Rukwa ni mkoa wenye fursa kubwa za kilimo, utalii na biashara. Serikali ya CCM itaendelea kuwekeza hapa ili wananchi wafaidike moja kwa moja na rasilimali zao,” amesema Samia.
Top of Form
Bottom of Form
Akizungumza kuhusu madini yanayochimbwa mkoani Rukwa ikiwemo makaa ya mawe, dhahabu na shaba, Samia amesema mkoa huo tayari umepokea wawekezaji 10 waliokwishaonyesha nia ya kuwekeza, na kwamba majadiliano bado yanaendelea.
“Serikali yetu itahakikisha wachimbaji wadogo wa ndani wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika sekta hii ya madini, ili wawe sehemu ya kunufaika na utajiri wa nchi yao,” amesema Samia.
Kuhusu sekta ya nishati, Samia amesema baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote nchini, hatua inayofuata ni kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme. Alisema ifikapo mwaka 2027, Tanzania itakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika, unaokatika tu kwa sababu za dharura za kiufundi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amewaomba wafanyabiashara wa ndani kuchangamkia fursa ya kuuza mahindi Malawi ambako mahitaji ni zaidi ya tani 200,000.
“Nendeni mkatafute masoko Malawi. Wamalawi na Wazambia wameshaanza kununua mahindi yetu. Msipowahi kuuza, NFRA itapelekwa kufanya biashara hiyo. Nawaambia wafanyabiashara wa Tanzania, acheni kuwa madalali wa wageni, nendeni mkauze wenyewe. Bei ya awali ni Dola za Marekani 280 kwa tani moja,” amesema Bashe ambaye pia ni Waziri wa Kilimo.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema Mkoa wa Rukwa umepiga hatua kubwa ya maendeleo, ukitoka kuwa mkoa wa pembezoni hadi sasa ukiwa na miundombinu bora ya barabara ikiwemo Tunduma hadi Sumbawanga.
“Kuhusu elimu, tuweke mkazo kwenye masomo ya sayansi ili tuweze kupata wataalamu watakaosaidia kuinua maendeleo ya eneo hili. Tukipata wasomi wa sayansi kutoka Rukwa, watakuwa chachu ya mabadiliko,” amesema Pinda.