Mchezo huo ni wa mwanzo katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo timu itakayosonga mbele itatinga hatua ya makundi.
Kabla ya mechi ya leo, Simba ilishinda mechi mbili zilizopita ilizocheza Eswatini ambazo ni dhidi ya Manzini Wanderers mwaka 1993 iliposhinda kwa bao 1-0 na mwaka 2018 iliposhinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Mbabane Swallows.
Bao la kwanza la Simba leo limepachikwa na Wilson Nangu katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.
Nangu alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Neo Maema baada ya mlinzi wa Nsingizini Hotspurs kuutoa mpira nje wakati alipokuwa katika harakati za kuuokoa.

Dakika saba kabla ya mpira kumalizika, Kibu Denis aliyeingia kutokea benchi, aliipatia Simba bao la pili kwa shuti la wastani la mguu wa kushoto akimalizia pasi nzuri ya kisigino ya Jonathan Sowah ambaye naye alianzia benchi.
Dakika ya 90 ya mchezo, Kibu alihitimisha karamu ya ushindi ya Simba baada ya kuifungia bao la tatu akimalizia pasi ya Morice Abraham.
Simba iliweza kulinda mabao yake na hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa, ilijihakikishia ushindi huo ambao unaipa mtaji mzuri katika mechi ya marudiano nyumbani Dar es Salaam, Jumapili ijayo.
Katika kipindi hicho cha pili, Simba mbali ya kumuingiza Sowah na Kibu, pia iliwapa nafasi Yusuph Kagoma, Morice Abraham na Chamou Karabou ambao walichukua nafasi za Wilson Nangu, Charles Ahoua na Joshua Mutale.

Kwenye Uwanja wa Intwari, Bujumbura, Burundi, Singida Black Stars imetoshana nguvu na wenyeji wao Flambeau du Centre kwa sare ya bao 1-1.
Matokeo hayo yanaifanya Singida Black Stars ihitaji ushindi wa aina yoyote au sare tasa nyumbani Jumapili ijayo ili iweze kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Bao pekee la Singida jana limefungwa na Clatous Chama.