Dar es Salaam. Mtihani wa ushindi wa kura za urais kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) umeachwa mikononi mwa waratibu wa kampeni za nafasi hiyo, waliogawanywa katika kila kanda.

Hatua hiyo ya CCM imeongeza chachu ya ushindani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Mbali na ule wa CCM dhidi ya vyama vya upinzani, pia kuna ushindani wa kanda moja dhidi ya nyingine za chama hicho tawala.

Jawabu la kanda ipi inayoongozwa na nani, ndiyo litakayokusanya kura nyingi za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, litajulikana baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 29, ingawa kila mratibu ameanza tambo akidai mikoa yake itakuwa kinara.

Mbiu za kuongoza kwa kura za urais kikanda zilianza kutolewa na Mratibu wa Kampeni za urais kupitia CCM katika Kanda ya Kati, Dk Bashiru Ally, aliyesema mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora ndio itaongoza kumpa kura mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan.

Msingi wa tambo za Dk Bashiru, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, ni idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kwenye mikutano ya kampeni za Samia iliyofanyika katika kanda hiyo.

Tambo za Bashiru

Dk Bashiru Ally amesema uongozi wa kanda yake kwa kura za rais utabebwa na maandalizi yaliyofanyika kwa ufanisi, utekelezaji mzuri wa ilani, mwitikio wa wananchi na mvuto wa mgombea urais.

Ameeleza mafanikio yanayoonekana katika kanda hiyo na maeneo mengine ya nchi ni matokeo ya kazi iliyofanywa na mgombea huyo, Samia.

“Kwa maandalizi tuliyonayo, mwitikio mkubwa wa wananchi na utekelezaji wa ilani ya chama, tutashinda kwa kura nyingi. Na baada ya uchaguzi, tathmini itaonesha kuwa Kanda ya Kati, ambayo ni Makao Makuu ya nchi, itaondoka kidedea.

“Nizipongeze Jumuiya ya Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake wa CCM. Hizi ndizo nguzo kuu za ushindi wa chama chetu. Ushindi si jambo la ghafla, ni matokeo ya kazi zao za kila siku,” amesema Dk Bashiru.

Ukiacha tambo hizo, kanda hiyo inahusisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, ambayo kwa ujumla ina wapigakura zaidi ya milioni 4.59. Katika mgawanyo huo, Mkoa wa Tabora una wapigakura milioni 1.799, Dodoma milioni 1.747 na Singida milioni 1.045.

Kanda ya Mashariki

Matumaini ya kura nyingi katika Kanda ya Mashariki yanatokana na historia yake katika uchaguzi uliopita, ikiwa ndiyo iliyoongoza kwa kura za rais, kama inavyoelezwa na Mratibu wa Kampeni za Rais wa kanda hiyo, Rajabu Abdallah.

Amesema anaamini kanda yake itaongoza kwa sababu uchaguzi mkuu uliopita mikoa yake (Pwani, Tanga na Morogoro) ilikaribiana kwa namba za juu za kura za urais.

“Tunachokifanya tutakwenda kutetea rekodi yetu kwa kuongeza nguvu. Lakini wenzetu, kwa kuwa hawana historia ya kuongoza, wanapokwenda kuanza, sisi tunaendelea tulipoishia,” amesema.

Matumaini mengine ya kuongoza katika kanda hiyo, Abdallah amesema yanabebwa na kiwango kikubwa cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/30 kilichofanyika katika mikoa ya kanda hiyo.

Amesema wanayoyazungumza ni yale yaliyofanyika, zaidi, kuna baadhi ya maeneo hayakutarajiwa kuguswa lakini yamefikiwa na utekelezaji wa ilani hiyo.

“Kwa sababu sisi tunakwenda hadi chini kuona kilichofanywa na Serikali kwa miaka mitano iliyopita na tumejiridhisha kwamba kweli kuna kazi imefanywa,” amesema Abdallah.

Siri nyingine ya kuongoza kwa wingi wa kura za rais katika kanda hiyo, kwa mujibu wa Abdallah, inatokana na umoja na ushirikiano ndani ya CCM kuanzia kwa viongozi na wanachama.

Kanda hiyo inahusisha mikoa ya Morogoro, Tanga na Pwani, yenye jumla ya wapigakura milioni 5.16. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mkoa wa Morogoro una wapigakura milioni 2.114, Tanga milioni 1.633 na Pwani milioni 1.413, ambao kwa ujumla ni milioni 5.16.

Kanda ya Ziwa

Akizungumza na Mwananchi, Mratibu wa Kampeni katika Kanda ya Ziwa, Aggrey Mwanri, amesema matumaini ya uongozi wa kura za rais katika kanda hiyo unatokana na mwamko uliooneshwa na wananchi katika mikutano ya kampeni za Rais.

Mikoa iliyokuwa inaratibiwa na Mwanri ni Geita, Shinyanga na Kagera.

Amesema amekuwa akifuatilia mikutano ya kampeni tangu zilipoanza, lakini katika mikoa ya kanda yake ndiko kulikokuwa na idadi kubwa ya wananchi kuliko maeneo mengine.

“Kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliojitokeza katika maeneo tuliyofanyia mikutano. Bila shaka idadi tulioongoza ndio tutakaoongoza kupiga kura,” amesema.

Mwanri amesema kazi kubwa imefanyika kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura, hivyo anaamini wamejiandaa vya kutosha kwenda kutekeleza haki hiyo.

“Tumepita kuwaomba wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura wafanye maandalizi, kujua kadi zao za kupigia kura zilipo, na waziandae ili siku ya uchaguzi waende kwa wingi kupiga kura,” amesema.

Kanda hiyo inahusisha mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera, ambayo kwa ujumla ina wapigakura milioni 4.541. Kwa mujibu wa INEC, Mkoa wa Geita una wapigakura milioni 1.532, Shinyanga milioni 1.244 na Kagera milioni 1.764.

Kanda ya Kusini

Mratibu wa Kampeni katika Kanda ya Kusini, Leyla Burhan Ngozi, amesema imani yake ya kuongoza kwa wingi wa kura inajengwa na mbinu walizozitumia kuwafikia wananchi wa mikoa yote ya kanda husika.

Ameeleza kwamba kabla ya ziara za wagombea na siasa za majukwaani, yeye kwa kushirikiana na wenzake walikwenda katika kila wilaya kuwasikiliza wananchi wanachokisema.

Kwa bahati nzuri, ameeleza kila walipokwenda wananchi walikiri kuridhishwa na utekelezaji wa ilani uliofanywa na mgombea na waliahidi kwenda kumpigia kura.

Sio hivyo tu, amesema hata katika mikutano yake na waratibu wenzake, kulijaa wananchi walioonesha matumaini kwa chama hicho na mgombea wake, huku msisitizo ukiwa kwamba watajitokeza kupiga kura.

“Kama wananchi wana mapenzi kiasi hicho na mgombea, na wenyewe wamesema wameridhishwa na kazi zilizofanyika, na wakaenda kupiga kura, naamini kanda yangu itaongoza kwa wananchi kujitokeza kupiga kura,” amesema Leyla, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Amesema kanda yake inahusisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, ambayo pia ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya wananchi, hivyo anaona kabisa wakiongoza.

“Tumefanya kampeni kubwa na tumefuata nyumba kwa nyumba, sio kwa wanachama wa CCM pekee bali hata kwa wale wasio wanachama, na wote wameahidi kwenda kupiga kura,” amesema.

Kanda hiyo inahusisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, yenye jumla ya wapigakura walioandikishwa na INEC milioni 3.16. Takwimu za INEC zinaonesha Mkoa wa Lindi una wapigakura 833,864, Ruvuma milioni 1.174 na Mtwara milioni 1.152.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *