
MICHUANO ya Swing ya Gofu ya Afrika Mashariki imewafuta vumbi la macho washiriki kutoka Tanzania ambao walifanya vizuri katika hatua za awali, lakini wakajikuta wakimaliza nyuma ya wale waliofanya vizuri zaidi.
Madina Iddi, ambaye amekuwa akishinda mashindano mengi ya kimataifa, alijikuta akimaliza katika nafasi ya sita kwa wachezaji wa ridhaa wenye viwango vya juu.
“Si vibaya sana kwa sababu lengo langu lilikuwa ni kumaliza katika 10-Bora nafasi ambayo hulipa sehemu ya Sh2 milioni za Kenya kama zawadi kwa washindi,” amesema Madina, anayetokea katika klabu ya Arusha Gymkhana.
Madina, hata hivyo amesema mashindano ya Swing ya Afrika Mashariki ni makubwa sana kwa sababu jumla ya malipo kama zawadi kwa washindi ni kama Sh400 milioni za Kitanzania na kivutio hiki cha zawadi ndiyo huchochea ushindani, kujituma na ajira.
Licha ya kufanikiwa kuingia katika orodha ya wachezaji 33 waliofuzu kucheza fainali za Swing ya Afrika Mashariki kwa wanaume, mambo hayakuwa mazuri sana kwa Watanzania wengine; Nuru Mollel, Isack Wanyenche na Isiaka Daudi ambao walishindwa kufikia lengo la 10-Bora.
Hawakuingia kumi bora kwa sababu walirudisha alama dhaifu, bali walioshinda walikuwa na alama zilizotukuka kwa ubora. Hata hivyo, cha kusisimua zaidi ni kwamba mshindi wa jumla alikuwa mchezaji gofu wa ridhaa, John Lejirma kutoka katika klabu ya Royal Nairobi Golf Club.
Lejirma, alimshinda mchezaji nguli wa kulipwa Njoroge Kibugu, katika hatua ya marudiano baada ya kumaliza na alama sawa.
Lerjima alishinda michuano kwa kupiga under 10, kiwango ambacho ni aghalabu kufikiwa kwa wachezaji wanaocheza katika ngazi isiyo ya PGA (Professional Golf Association) ambayo ni maalum wa wachezaji wa kulipwa wa kimataifa.
“Kwa mashindano ya Tanzania, wachezaji wengi wanashinda michuano kwa kiwango +4 au +5 katika mashindano ya mashimo 54, lakini under 10 ni nadra sana kufikiwa,” alifafanua Mollel.
Moja ya matokeo ya kutisha ni mikwaju 66 aliyoitengeneza mchezaji Njoroge, kwani ilizidi kiwango cha uwanja kwa mikwaju 6.
Kwa kushinda nafasi hiyo, Kibugu aliondoka na kitita cha Sh214,000 za Kenya (sawa Sh4 milioni za Tanzania).