Rais Donald Trump wa Marekani amebadilisha ghafla msimamo wake wa kutuma makombora ya cruise ya Tomahawk kwenda Ukraine.
Inaonekana kwamba masuala ya jiografia ya kisiasa, tahadhari za kijeshi, na mwingiliano wa kidiplomasia na Russia na Ukraine vimehusika katika mabadiliko haya.
Televisheni ya CNN imeripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, alibadili mawazo yake kuhusu kuunga mkono mashambulizi ya Ukraine kwenye vituo vya nishati vya Russia baada ya kuzungumza na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin, lakini amebakisha mezani chaguo la kutuma makombora ya Tomahawk nchini Ukraine. Baadhi ya wachambuzi pia wanaamini kwamba, Trump hajabadilisha kabisa msimamo wake kuhusu suala hili, bali yuko kwenye hatihati ya kufanya uamuzi wa mwisho na anapima kwa uangalifu matokeo ya hatua za kidiplomasia, kijeshi na kiufundi ya hatua hiyo. Pamoja na hayo, ushahidi unaonyesha kuwa Trump amebadili mawazo yake kuhusu kutuma makombora ya Tomahawk nchini Ukraine.

Hata hivyo inaonekana kuwa, kuna mambo yafuatayo nyuma ya uamuzi wa Trump:
Kwanza ni wasiwasi kuhusu kuongezeka mvutano na Russia. Moja ya sababu kuu za mabadiliko ya msimamo wa Trump ni wasiwasi wa kuzidisha moja kwa moja mzozo na Russia. Trump anafahamu vyema kwamba Moscow imetangaza kwamba kutumwa makombora ya Tomahawk huko Ukraine ni mstari mwekundu katika uhusiano wa Russia na Marekani. Kwa hivyo, baada ya mazungumzo ya simu na Rais wa Vladimir Putin, Trump alitangaza kuwa yuko tayari kutupilia mbali uungaji mkono wa moja kwa moja kwa mashambulio ya Ukraine kwenye miundombinu ya Russia. Hata hivyo amebakisha mezani chaguo la kutuma makombora ya Tomahawk huko Ukraine na anaendelea kulishikilia kama chombo cha mashinikizo ya kidiplomasia.
Pili ni tahadhari kuhusu kudumisha nguvu za kijeshi za Marekani: Trump amesisitiza kuwa Tomahawk ni silaha zenye nguvu sana, na kwamba Marekani lazima iwe na tahadhari katika kuzitumia. Ameashiria matumizi ya makombora 30 ya Tomahawk katika shambulizi dhidi ya Iran na kusema kuwa Marekani inayahitaji makombora hayo na haipaswi kuyatoa kwa wengine kirahisi. Suala hili linaakisi hamu ya Trump ya kudumisha mlingano wa nguvu na uwezo wa kijeshi kwa kiwango cha kimataifa.

Tatu ni changamoto za kiufundi na kilojistiki: Mojawapo ya vizingiti vya kivitendo ni jinsi ya kurusha makombora hayo. Kimsingi, Tomahawk ni silaha ya jeshi la majini, na Ukraine ingehitaji kujenga vituo vya nchi kavu kwa ajili ya kurushia makombora hayo. Vilevile, ugavi wa makombora haya kwa ajili ya kupelekwa Ukraine unaweza kuwa mdogo, kwa sababu sehemu ya akiba ya Tomahawk imetengwa kwa ajili ya misheni ya Jeshi la Marekani.
Nne ni kutumia vitisho kama karata ya mazungumzo. Katika mazungumzo ya simu na Zelenskyy, Trump alitangaza kwamba anaweza kumpa Putin kauli ya mwisho: “ikiwa Russia haitarejea kwenye mazungumzo ya amani, Marekani itaipatia Ukraine makombora ya Tomahawk”. Tishio hili linaonyesha kuwa Trump anatumia chaguo la kutuma makombora ya Tomahawk huko Ukraine kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa ili kulazimisha Russia kufanya mazungumzo, na sio kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Tunahitimisha uchambuzi wetu huu kwa kusema kuwa, kubadilika msimamo wa Trump kuhusu suala la kutuma makombora ya Tomahawk nchini Ukraine ni matokeo ya mseto wa masuala ya kidiplomasia, kijeshi na kisiasa. Trump anajaribu kutumia wenzo huu wenye nguvu kama chombo cha kumaliza vita, bila kuingia moja kwa moja kwenye mzozo au kuhatarisha rasilimali za kijeshi za Marekani.