Dar es Salaam. Mgombea udiwani wa Kata ya Kunduchi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Michael Urio amesema ataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wananchi wa Kunduchi, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, wanawezeshwa kiuchumi kupitia mikopo na mpango wa bima ya afya kwa wote.

Amesema ndani ya siku 100 zijazo, atahakikisha kupitia ushirikiano na serikali, biashara zote ndogo ndogo za eneo hilo zinakuwa zimesajiliwa rasmi ili wajasiriamali wadogo waweze kunufaika na fursa za kifedha na mikopo.

“Kama wewe ni bodaboda, bajaji, mamalishe, au mfanyabiashara wa mboga mboga biashara zako zitarasimishwa. Hii itawawezesha kupata mikopo na huduma za kibenki kwa urahisi,” amesema.

Akizungumza leo Jumapili Oktoba 19, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtongani, Kata ya Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Urio amesema zaidi ya Sh310 milioni zimetolewa kwa vikundi mbalimbali vya wananchi kama sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan.

Wananchi wa Kunduchi wakimsikiliza mgombea udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Michael Urio

Amesema katika eneo la Kilongawima, kikundi cha wanawake watano kimepata mkopo wa Sh100 milioni, ambao umewezesha kuanzishwa kwa kiwanda kidogo cha uzalishaji.

Ameongeza kuwa katika eneo la Kondo, kikundi cha vijana kimepata zaidi ya Sh80 milioni na kimeanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu, pia vijana wengine wamepatiwa Sh130 milioni kwa ajili ya mradi wa utengenezaji wa bidhaa za plastiki.

“Hapa Kunduchi pia tuna kikundi cha wanawake waliopata zaidi ya Sh 30 milioni kwa ajili ya mradi wa kufyatua tofali. Serikali ya Samia imejipambanua kwa vitendo katika kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi,” amesema Urio.

Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia chama hicho, Geofrey Timoth amesema utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote, utamaliza changamoto ya wananchi wengi kushindwa kupata huduma bora za matibabu na kuondoa tatizo la watu kuzuiliwa maiti hospitalini kutokana na ukosefu wa fedha.

“Tafsiri yake ni kwamba bima nitakayokuwa nayo mimi mbunge na diwani, ndio atakayokuwa nayo mwananchi wa kawaida wa Kunduchi. Hii itamaliza kabisa tatizo la watu kuzuiliwa maiti hospitalini kwa sababu ya ukosefu wa fedha,” amesema Timoth.

Timoth amesema serikali ya CCM itaendelea  kuboresha sekta ya elimu kwa kupunguza michango shuleni, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora bila kikwazo cha kifedha.

“Najua wazazi mmekuwa mkikwazwa na michango mashuleni, lakini serikali inachukua hatua kuhakikisha elimu inapatikana bure na kwa ubora zaidi,” amesema.

Amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya shule na kuongeza ujenzi wa madarasa, ili kuwezesha watoto wote kusoma katika mazingira mazuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *