Kishapu. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Watanzania hawana sababu ya kusita kumpa tena miaka mingine mitano Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa alizozifanya katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake.

Akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, Wasira amesema miradi mikubwa iliyotekelezwa ikiwemo Reli ya Kisasa ya Kiwango cha Kimataifa (SGR), Bwawa la Mwalimu Nyerere na Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi) ni uthibitisho wa uwezo, ujasiri na uongozi makini wa Rais Samia.

“Mradi wa SGR umefika Makutupora kwa zaidi ya kilomita 700 kutoka Dar es Salaam, na kazi inaendelea kutoka Mwanza hadi Kigoma. Huu ni ushahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka nguvu kubwa kuhakikisha miundombinu inaimarika,” amesema.

Akimzungumzia zaidi Rais Samia, Wasira amesema amesimamia miradi aliyoachiwa na mtangulizi wake, hayati John Magufuli, ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo sasa limekamilika na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

“Sasa hivi nchi ina umeme wa kutosha. Wakati Magufuli anaondoka, bwawa lilikuwa asilimia 30; ndani ya miaka minne ya Rais Samia limekamilika. Huo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuhakikisha kazi inaendelea,” amesisitiza Wasira.

Akizungumzia Daraja la Magufuli lililopo Kigongo–Busisi, Wasira alisema limeondoa usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakitumia muda mrefu kuvuka kwa vivuko, na sasa safari hiyo inachukua dakika chache tu.

Akimhitimisha hotuba yake, Wasira amesema Rais Samia ameonesha kipawa cha uongozi na busara za hali ya juu katika kusimamia nchi, licha ya kuchukua madaraka katika mazingira magumu.

“Urais si jambo la ghafla. Ni matokeo ya maandalizi, sheria, kanuni na busara. Hakuna ushahidi kwamba wanaume wana busara zaidi ya wanawake. Rais Samia amebarikiwa kipawa cha uongozi na amethibitisha kuwa anaweza,” amesema.

Ameongeza, “Kazi imeendelea, na sasa jukumu letu ni moja tujitokeze kwa wingi kumpa heshima anayostahili kwa kumpigia kura Samia katika uchaguzi ujao. Mitano tena ni ya kazi zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *