Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amekutana na mwenzake wa Liberia, Sara Beysolow Nyanti kujadili njia za kupanua ushiriki wa Marekani katika sekta muhimu ya madini nchini Liberia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott ametangaza katika taarifa yake kwamba Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Liberia, Marco Rubio na Sara Beysolow wamekutana ili kujadili suala la kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kupanua ushiriki wa kibiashara wa Washington katika nchi hiyo ya Kiafrika. Imeelezwa kuwa, mkutano huo ulijadili njia za kupanua ushiriki wa Marekani katika sekta muhimu ya madini nchini Liberia kwa lengo eti la kutayarisha nafasi za kazi na ukuaji wa uchumi katika nchi zote mbili.
Afrika, haswa katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, imekuwa kitovu muhimu cha kudhamini madini ya thamani ikiwa ni pamoja na madini yanayohitajika viwandani. Rasilimali hizo za madini ni pamoja na metali adimu, dhahabu, almasi, cobalt, lithiamu na shaba, ambazo hutumika katika uzalishaji wa teknolojia za kisasa, magari ya umeme na hata zana za kijeshi. Mahitaji haya yanayoongezeka ya madini, hasa wakati dunia ikielekea kwenye nishati jadidika, na kupungua utegemezi kwa nishati ya fosili, vimezidisha umuhimu wa kutafuta rasilimali za madini za bara la Afrika.
Ijapokuwa Marekani imekuwa ikilipa umuhimu suala la kuwepo katika nchi mbalimbali za Afrika kwa miongo kadhaa, na ina kambi nyingi za kijeshi katika nchi mbalimbali barani hilo, lakini katika muongo uliopita, utajiri wa rasilimali za madini za Afrika umevutia hisia za nchi mbalimbali hususan Marekani, ikiwa ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa rasilimali hizo. Kwa sababu hiyo, Marekani inaimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika, hasa nchi tajiri kwa rasilimali za madini kama Liberia.
Marekani inajaribu kupanua ushirikiano wake katika uchimbaji na usindikaji wa madini katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kisingizio cha kusaidia maendeleo ya kiuchumi. Lakini hii siyo sababu pekee ya Marekani kukodolea macho rasilimali za madini za Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, China, ikiwa ni mshindani mkuu wa Marekani kiuchumi, imeimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika. Kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini na miundombinu, China imekuwa mojawapo ya washirika wakuu wa biashara wa nchi za Afrika. Mahusiano haya yamepanuka sana, haswa katika uwanja wa madini yanayotumika katika tasnia ya teknolojia na nishati mbadala. Marekani pia inataka kuimarisha nafasi yake katika ushindani na China na nchi nyingine zinazostawisha uhusiano wa kibiashara na Afrika.

Ingawa Marekani sasa imeingia katika mazungumzo na kufunga mikataba na nchi nyingi za Afrika katika fremu ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, lakini upande wa pili wa ushirikiano huu pia ni muhimu. Kwa msingi huo, iwapo nchi za Kiafrika hazitaingia katika njia hiyo kwa ufahamu, moyo wa kutaka kujitawala na uhuru, wimbi jipya la wakoloni litaingia katika nchi za bara hilo, mara hii katika mundo na sura ya mikataba ya kiuchumi. Unyonyaji wa vibarua na nguvu kazi ya bei nafuu, mishahara duni, na kutozingatia sheria za kulinda mazingira katika sekta ya madini ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo viongozi wa nchi za Afrika wanapaswa kuyashughulikia.
Kutokuwepo miundombinu inayofaa na taasisi madhubuti za udhibiti katika nchi nyingi za Afrika, vimekuwa sababu ya kutumiwa maliasili za bara hilo bila kuzingatia umuhimu wa mazingira na masuala mengine muhimu ya kijamii. Vilevile, baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaeleza kuwa makampuni ya kigeni, hasa katika sekta ya madini, yanaweza kutumia mazingira ya kikatili ya kufanyia kazi kwa ajili ya kuchimba rasilimali hizo, huku manufaa ya uchimbaji huo yakibaki mikononi mwa kundi la watu wachache kwa njia isiyo ya kiadilifu. Kwa sababu hiyo, baadhi ya nchi na mashirika ya kimataifa yanatoa wito wa kuwepo uwazi zaidi katika sekta hii na kuheshimiwa viwango vya mazingira na haki za binadamu.
Ukweli ni kwamba, katika dunia ya sasa ambapo ushindani wa kuwania rasilimali muhimu unazidi kuongezeka siku baada ya siku, Afrika imekuwa uwanja wa kimkakati kwa wachezaji wakuu kwenye medani ya masuala ya kiuchumi na kisiasa.
Kwa sasa, Marekani ikitumia kauli mbiu ya kuimarisha maendeleo na kutengeneza nafasi za ajira, inataka kuthabitisha ushawishi wake katika nchi za Afrika ambazo bado zina makovu ya ukoloni mkongwe. Hivyo, iwapo nchi za Afrika hazitaweza kusimama imara dhidi ya wimbi hili jipya la wakoloni kwa mwamko, uhuru, na utashi wa kisiasa, kwa mara nyingine tena ukoloni mamboleo utaweka kivuli juu ya hatima ya bara hilo, lakini mara hii si kwa kutumia mtutu wa bunduki, bali kwa mikataba ya kibiashara, mashirika ya kimataifa, na ahadi za kuleta maendeleo.