Kuna uwezekano mkubwa Azam FC ikatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kutokana na matokeo iliyopata katika mechi ya ugenini ya raundi ya pili dhidi ya KMKM ya Zanzibar, juzi Jumamosi.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao Azam FC iliupata, unaifanya ihitaji matokeo angalau ya sare ili iweze kuingia hatua ya makundi lakini hata ikipoteza kwa tofauti ya bao moja pia itasonga mbele.

Na ikifanikiwa kuingia hatua hiyo, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza hatua ya makundi sio tu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika bali pia hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika tangu ilipoanzishwa mwaka 2004.

Timu hiyo kuanzia mwaka 2008 iliposhiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza, imekuwa ikipambana vilivyo kuhakikisha inaingia hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, lakini mara kwa mara ilikuwa ikigonga mwamba.

Zipo nyakati kadhaa ambazo ilikaribia kuingia katika hatua hiyo lakini katika dakika za lala salama ilikwama ama kutokana na ubora wa wapinzani wao au makosa machache ya wachezaji wake.

Mashabiki wa Azam FC na Watanzania wapenda soka hapana shaka watakuwa na kumbukumbu ya mwaka 2013 ambapo Azam FC ilikwamia katika raundi ya pili mbele ya FAR Rabat ya Morocco baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 katika mechi mbili baina ya timu hizo.

Katika mchezo wa kwanza, Azam FC ilitoka sare ya bila kufungana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na ziliporudiana huko Morocco, wawakilishi hao wa Tanzania walipoteza kwa mabao 2-1.

Azam FC ilikuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kwani katika mechi hiyo ya marudiano ugenini, ilipata mkwaju wa penalti katika dakika za lala salama ambao kama ingefungwa, mchezo ungemalizika kwa sare ya mabao 2-2 na hivyo ingesonga mbele kwa faida ya bao la ugenini lakini kwa bahati mbaya, John Bocco alikosa tuta hilo na hivyo kufanya timu yake itolewe mashindanoni.

Pamoja na yote, uongozi wa Azam FC uliendelea kuwa na uvumilivu na imani kwamba siku moja timu yao itategua kitendawili ambacho kimekuwa kikiipa shida kutoa majibu na kuingia katika hatua ya makundi.

Katika mahojiano mbalimbali na vyombo vya habari, viongozi wa Azam FC walikuwa wakisisitiza kwamba mafanikio ni mchakato na wao hawakatishwi tamaa na kushindwa kwao kupenya hadi hadi hatua ya makundi bali wanatumia hilo kama darasa la kujiimarisha zaidi ili siku moja nao waingie katika vitabu vya kihistoria kutinga katika hatua hiyo au zaidi.

Inawezekana walikuwa wakiumia kuona timu ndogo kama Namungo FC ikifanikiwa kuingia katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla yao lakini bado walisimama imara na kuonyesha kuwa wanaamini katika njia wanayopita hata kama bado matunda yanachelewa kuonekana.

Hawakuacha kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika ujenzi wa kikosi chao, maandalizi ya timu pamoja na kugharamia benchi la ufundi katika kila msimu na hatimaye sasa mwanga unaanza kuonekana.

Japo mpira wa miguu huwa na matokeo ya kushangaza, ni ngumu kuamini kwamba KMKM inaweza kupindua matokeo ya kichapo cha mabao 2-0 ambacho imekipata katika mechi ya kwanza hivyo kwa hesabu za haraka haraka, Azam FC tayari ina nafasi kubwa kwenye makaratasi kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Daraja la uvumilivu lililoonyeshwa na uongozi wa Azam FC katika miaka 17 ambayo timu hiyo imekuwa ikishiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara linaweza kuwa somo zuri kwa viongozi wa wadau wa soka nchini kuwa mpira wa miguu ni mchezo ambao mara kwa mara unahitaji subira hasa katika nyakati za kuyakimbilia mafanikio.

Kama uongozi wa Azam FC usingekuwa na uvumilivu, pengine baada ya majaribio kadhaa ya kuingia hatua makundi yalipokwama, ungeamua kutoendelea kupoteza kiasi kikubwa cha fedha katika uendeshaji wa timu hiyo na kuamua kukielekeza katika masuala mengine.

Lakini wenyewe ndio ukawa unazidi kuongeza kiasi cha fedha katika bajeti ya uendeshaji wa timu huku ukiamini kwamba palipo na giza nene, mwanga unakaribia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *