BAADA ya kuambulia sare ya bao 1-1 ugenini, Kocha mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema bado ana dakika 90 ngumu za kuandika rekodi ya kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku akiweka wazi bao moja la ugenini ni mtaji mkubwa.

Singida Black Stars itakuwa mwenyeji kwenye mechi ya marudiano ya kuamua hatma ya nani kutinga hatua ya Makundi ya michuano hiyo dhidi ya Flambeua FC, itakayochezwa Oktoba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Dar baada ya ule wa ugenini uliochezwa juzi Jumapili, kutoka sare na Clatous Chama alianza kuifungia Singida dakika ya 54 kabla ya Flambeau kusawazisha dakika ya 59 kwa bao la Edson Munaba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi amesema wamesahau matokeo yaliyopita licha ya kuwa na faida kwao, sasa wanajiandaa kwa dakika nyingine 90 ngumu nyumbani.

“Haikuwa rahisi licha ya wachezaji wangu kuonyesha mchezo mzuri, makosa machache yametugharimu, tunajipanga kwa mchezo unaofuata tukiwa nyumbani tutaingia kwa kumuheshimu mpishani lakini pia kuhakikisha tunaandika rekodi mpya.

GAMO 01

“Wapinzani wetu ni bora lakini sisi pia ni bora zaidi najivunia wachezaji wangu wote nilionao wana uzoefu licha ya kutanguliwa hawakuonyesha kukubali walipambana na baadae tulipata bao ambalo limetufanya turudi na nguvu.”

Gamondi amesema dakika 90 za nyumbani ni ngumu zaidi ya zilizopita, hivyo wanahitaji kujiandaa vizuri ili kufikia mipango yao huku akisisitiza kuwa bado wana kazi ya kufanya kutokana na kucheza dhidi ya timu ambayo inahitaji nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

“Napewa nguvu na wachezaji wangu wana utayari wa kufikia malengo na wamenihakikishia kuwa tuna nafasi ya kufuzu hatua inayofuata, hivyo kazi yangu ni kusuka mipango mikakati imara, utayari wa wachezaji ndio itakuwa chachu yetu,” amesema.

Akizungumzia michuano hiyo kwa jumla, amesema inahitaji utayari na uwekezaji mkubwa kwa kuunda kikosi shindani kitu ambacho ameweka wazi tayari kipo kwenye timu yake.

GAMO 02

“Uwekezaji na utayari ndio siri kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hii ya kimataifa, naona Singida Black Stars ikifanya vizuri hasa tukifanikiwa kutinga hatua ya makundi mchezo wetu wa nyumbani wachezaji wangu wana utayari na nina bahati kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wazoefu,” amesema.

Katika kikosi cha Singida Black Stars, kuna Khalid Aucho na Chama ambao msimu uliopita 2024-2025 walifuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakifundishwa na Gamondi.

Singida Black Stars katika mechi ya marudiano, inahitaji matokeo ya 0-0 au ushindi wa aina yoyote ili kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *