Liverpool, England. Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, amemwambia kocha wa sasa Arne Slot kwamba wakati umefika Mohamed Salah asiwe tena mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool, kufuatia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Manchester United kwenye dimba la Anfield.
Carragher amesema Salah, ambaye kwa miaka mingi amekuwa nguzo kuu katika safu ya ushambuliaji ya Liverpool, sasa anatakiwa kusimamiwa kwa umakini zaidi kwani ushawishi wake umeanza kupungua.
“Ni changamoto kubwa kwa kocha. Ni jambo la kuvutia kwamba alimtoa nje. Hata wakati wa Klopp, Salah alikuwa akitolewa mara kwa mara, na hiyo ilionyesha kwamba hata kama alikuwa na nguvu, kulikuwa na nyakati alizokuwa na mechi mbaya,” amesema Carragher kupitia Sky Sports.
“Tuko kwenye hatua sasa ambapo Mo Salah hapaswi kucheza kila mechi. Si lazima kila wakati awe jina la kwanza kwenye kikosi. Anaweza kucheza mechi za nyumbani, lakini si lazima acheze zote, hasa kama Liverpool ina mechi mbili mfululizo, moja Ulaya na nyingine ugenini. Slot anatakiwa kuwa makini hapo.”
Kauli hiyo imekuja wakati Liverpool ikipoteza mechi ya nne mfululizo katika michuano yote, na tatu kati ya hizo zikiwa za Ligi Kuu England. Kikosi cha Slot, ambacho mwezi uliopita kilikuwa kinangoza ligi kwa alama tano, sasa kimeshuka hadi nafasi ya tatu, pointi nne nyuma ya vinara Arsenal.
Katika mechi hiyo ya Anfield, Bryan Mbeumo aliwapa United uongozi ndani ya sekunde 62 kufuatia makosa ya Virgil van Dijk na Alexis Mac Allister, kabla ya Cody Gakpo kusawazisha kipindi cha pili. Hata hivyo, kichwa cha Harry Maguire dakika za mwisho kiliihakikishia United ushindi wao wa kwanza Anfield tangu mwaka 2016.
Naye beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, naye ametoa maoni yanayofanana na ya Carragher kuhusu Salah, akisema anaanza kuona dalili za kushuka kiwango si kwa mwili, bali kiufundi.
“Kuna maswali mengi juu yake sasa, labda ni msimu mmoja zaidi kupita kiasi. Lakini cha kushangaza ni kwamba si kushuka kwa kasi au nguvu, kwa sababu anaonekana bado yuko fiti,” amesema Neville kupitia Gary Neville Podcast.
“Kinachonishangaza ni upande wa kiufundi. Vile anavyopiga krosi au kuchukua mipira kwenye eneo la nyuma ya goli hiyo haikuwa kawaida yake. Kuna nyakati alikuwa akipiga vibaya kabisa, kitu ambacho kwa Mo Salah ni ajabu.”
Neville pia alikosoa safu ya ulinzi ya Liverpool, akisema ilicheza “vibaya mno” na “bila mpangilio”.
“Van Dijk hakuwa kwenye ubora wake kabisa, Kerkez upande wa kushoto bado hajazoea, anaonekana kama beki chipukizi wa miaka 10. Bradley upande wa kulia alikuwa wa wastani, lakini kwa ujumla walikuwa wabovu sana leo,” amesema nyota huyo wa zamani wa United.
Liverpool sasa inaelekea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Eintracht Frankfurt katikati ya wiki kabla ya kurejea kwenye ligi dhidi ya Brentford, wakiwa na jukumu zito la kuzuia mwenendo mbaya unaoweza kuharibu kabisa matumaini yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.