Uganda. Mkongwe wa muziki Jose Chameleon kutokea nchini Uganda amekata mzizi wa fitina kuhusiana na Juliet Zawedde aliyekuwa akihusishwa kutoka naye kimapenzi baada ya mwanadada huyo mjasiriamali wa Uganda anayeishi Marekani kufunga ndoa na staa wa Bongofleva, Maximillian Rutta ‘Bushoke’ ambaye ni rafiki wa Chameleon.
Kabla ya Juliet kufunga ndoa na Bushoke alimsaidia Chameleon wakati anaugua, jambo lililowafanya watu wawahusishe mapenzi, kitu ambacho amekuja kukiona staa huyo kutoka Uganda.
Chameleon alikwenda kuhudhuria harusi ya wawili hao iliyofungwa nchini Marekani na alipopewa nafasi ya kusema neno ndipo alipofichua kuwa anampenda mrembo huyo kama dada yake na siyo jambo jingine.
“Kama mnadhani naweza kuwa na wivu na Juliet mtakuwa mnapoteza muda, Bushoke namchukulia kama ndugu kwa maana ya kaka na Juliet kama dada nampenda sana kwani ana utu na kujali changamoto za wengine,” amesema Chameleon na kuongeza;

“Nakushukuru sana Bushoke una moyo wa kipekee hata wakati naumwa ulikuja Marekani kuniona, hivyo taarifa za mitandaoni kunihusishwa na Juliet zimefika mwisho wake.”
Bushoke na Chameleon waliwahi kufanya wimbo wa pamoja uliyojulikana kwa jina la Mama Rhoda, hivyo wanafahamiana kitambo.
Ndoa hiyo ilihudhuriwa na wageni wachache, akiwamo msanii Jose Chameleone, ilifungwa Oktoba 17, 2025 nchini Marekani kwenye jimbo la Massachusetts.
Akizungumza kwa WhatsApp call Bushoke ameliambia Mwananchi kuwa, ameamua kutimiza ndoto yake ya kufunga ndoa ambayo alikuwa nayo muda mrefu kuwa ipo siku atakuja kufunga ndoa na mwanamke anayempenda.

“Nashukuru sana kutimiza ndoto yangu, ndoto ambayo nilikuwa naiota kila uchao kuwa nitakuja kufunga ndoa na mwanamke ambaye nampenda, hivyo nimempata mke wangu Juliet mwanadada wa Uganda, ambaye ni mjasiriamali anayeishi Marekani”
“Na uzuri ni mwanamke ambaye ni rafiki mkubwa wa rafiki yangu Jose Chameleone, hivyo imekuwa ni furaha sana kwetu sote kuwa familia moja”, amesema Bushoke.
Miezi saba iliyopita, Bushoke alilitonya Mwananchi kuwa, yupo nchini Marekani, ambako alienda kwa mwaliko wa Jose Chameleon kwa ajili ya kazi.
Bushoke amesema urafiki wao wa muda mrefu ulizaa matunda na anapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Chameleon.

“Nipo naye hapa Boston, Marekani. Yeye ndiye amenialika mpaka hapa nilipo, kila kitu ni yeye, hata hii connection mpaka hii interview tunayofanya sasa hivi, yeye yupo nyuma,” amesema Bushoke miezi saba iliyopita.
Bushoke amemshukuru Chameleon kwa upendo wake, akisema wamekuwa marafiki kwa takriban miaka 20.