Gavana wa Darfur, magharibi mwa Sudan, Minni Arko Minawi, amesema kuwa mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) dhidi ya El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, ni sawa na mauaji ya halaiki.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Sudan, Minni Minawi ameshutumu kile alichokiita wanamgambo waasi, akiwa na maana ya Vikosi vya Msaada wa Haraka, na mashambulizi yake yanayolenga mikusanyiko ya kiraia ya wanawake na watoto.

Siku ya Jumamosi, vyanzo vya kijeshi katika kikosi kinachoshirikiana na jeshi la Sudan, vilitangaza kwamba vimezima shambulio kubwa la nchi kavu lililoanzishwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka kwenye mji wa El Fasher, Darfur Kaskazini, huko magharibi mwa Sudan.

Shambulio hilo la RSF liliambatana na risasi za mizinga zilizolenga vitongoji kadhaa vya makazi ya watu waliohamishwa ndani ya mji, ambao umezingirwa tangu Mei 2024.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa jeshi na vikosi vya washirika vilisababisha hasara kubwa kwa wapiganaji na vifaa vya waasi.

Serikali ya Sudan na mashirika ya ndani na ya kimataifa yanalituhumu kundi la RSF  kuwa limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye maeneo ya makazi ya raia huko El Fasher na kambi za wakimbizi.

Vikosi vya Msaada wa Haraka vimekuwa vikiuzingira mji wa El Fasher tangu Mei 2024, na licha ya mashambulizi ya mara kwa mara, vimeshindwa kuvunja ulinzi wa Kitengo cha 6 cha Jeshi la Sudan kinacholinda mji huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *