
Hitilafu iliyotokea katika huduma za Amazon Web Services (AWS) leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 imesababisha usumbufu mkubwa katika mtandao, ikiathiri mamia ya programu na tovuti maarufu duniani kote.
Huduma kama Snapchat, Canva, Venmo, Duolingo, Coinbase, Fortnite na Roblox zimepata changamoto za kushindwa kufunguka, utendaji wa taratibu au kukatika kabisa kwa muda.
Kwa mujibu wa tovuti ya Downdetector, zaidi ya taarifa 50,000 za kukatika kwa huduma ziliripotiwa muda mfupi baada ya saa 1:50 asubuhi leo, watumiaji wakielezea matatizo ya muunganisho, uchelewaji wa majibu na kukosekana kabisa kwa huduma.
Hitilafu hiyo pia imeathiri huduma za Amazon yenyewe, zikiwamo Alexa na programu yake ya ununuzi kupitia simu.
AWS ilikiri kuwepo kwa hitilafu hiyo, ikibainisha kuwa, kulikuwa na ongezeko la makosa katika huduma kadhaa, na ikathibitisha kuwa juhudi za kurejesha huduma zilikuwa zinaendelea.
AWS imesema imekutana na ongezeko la viwango vya juu vya makosa na ucheleweshaji wa huduma, katika huduma kadhaa.
“Tunaendelea kufanya kazi kupitia njia kadhaa kwa wakati mmoja ili kuharakisha kurejesha huduma,” inaeleza taarifa yake.
Hitilafu hii ya AWS ndiyo usumbufu mkubwa wa kwanza wa kimtandao tangu tukio la mwaka jana la ‘CrowdStrike’, lililotatiza mifumo ya kiteknolojia katika hospitali, benki na viwanja vya ndege duniani kote.
AWS hutoa huduma za kompyuta kwa mahitaji (on-demand computing power), hifadhi ya data na huduma nyingine za kidijitali kwa kampuni, Serikali na watu binafsi.
Mvurugiko katika seva zake unaweza kusababisha tovuti na majukwaa mengi kushindwa kufanya kazi, kwa kuwa mengi yanategemea miundombinu yake ya kuhifadhi dara. AWS inashindana na huduma za hifadhi data za Google na Microsoft.
AWS ilielekeza mashirika habari kwenye ukurasa wake wa taarifa za huduma (status page) ilipoombwa kutoa maoni, huku Amazon yenyewe ikishindwa kujibu maombi ya kutoa maoni yao kuhusu kilichotokea.
Kampuni ya ‘Akili Unde’ (AI startup) iitwayo Perplexity, soko la fedha za kidijitali Coinbase na programu ya biashara ya hisa Robinhood, zote zilitaja AWS kuwa chanzo cha matatizo hayo.
“Mfumo wa Perplexity haupo hewani kwa sasa. Sababu kuu ni hitilafu katika AWS. Tunaendelea kushughulikia tatizo hilo,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Perplexity, Aravind Srinivas, kupitia mtandao wa X.
Tovuti ya ununuzi ya Amazon, huduma ya Prime Video na kifaa cha sauti cha Alexa pia zimepata matatizo, kwa mujibu wa tovuti ya Downdetector.
Miongoni mwa majukwaa ya michezo ya mtandaoni yaliyoathirika ni Fortnite (inayomilikiwa na Epic Games), Roblox, Clash Royale na Clash of Clans.
Vivyo hivyo, majukwaa ya kifedha kama Venmo na Chime (yanayomilikiwa na Paypal) nayo yamepata hitilafu, kwa mujibu wa taarifa za Downdetector.
Programu ya usafiri Lyft, mpinzani wa Uber, pia imeshindwa kufanya kazi na kukwamisha maelfu ya watumiaji nchini Marekani.
Rais wa programu ya ujumbe ‘Signal’, Meredith Whittaker, amethibitisha kupitia mtandao wa X kwamba jukwaa lao pia liliathiriwa na hitilafu ya AWS.
Nchini Uingereza, benki za Lloyds Bank, Bank of Scotland na kampuni za mawasiliano Vodafone na BT pia zimekumbwa na matatizo hayo, kwa mujibu wa tovuti ya Downdetector UK.
Tovuti ya mamlaka ya kodi, malipo na ushuru wa forodha (HMRC) nchini Uingereza pia imepatwa na hitilafu kutokana na tatizo hilo.