HADITHI fupi ya Kocha Romain Folz klabuni Yanga imefikia tamati baada ya Mfaransa huyo kuondoka Jangwani kwa makubaliano ya pande mbili, lakini mwanzo wa mwisho wake ulionekana mapema zaidi.

Tangu msimu huu Yanga ilikuwa ikicheza soka tofauti na mashabiki wa timu hiyo walivyoizoea na licha ya kupoteza mechi moja tu na kuruhusu bao moja katika sita ilizocheza, ushindi ulionekana ukitegemea zaidi vipaji binafsi vya baadhi ya mastaa wake akiwamo Pacome Zouzoua.

Ndiyo maana katika mechi ambayo Pacome alibanwa, haikushangaza kuona timu hiyo ikipoteza mchezo wake wa ugenini Malawi dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, Silver Strikers.

Huku mshambuliaji nyota Clement Mzize mwenye uwezo wa kuwapunguza mabeki na kufunga akiwa nje ya uwanja kutokana na majeraha, Yanga imeonekana kupoteza makali mbele.

Hata nafasi za kufunga hazionekani kutengenezwa kwa wingi tangu alipoondoka Stephane Aziz Ki aliyejiunga na Wydad Cassablanca ya Morocco wakati pia Yanga haionekani kutawala eneo la kiungo ambalo pia lilikuwa likianzisha mashambulizi mengi kabla ka kuondoka kwa Khalid Aucho ambaye kati ya sifa zake kubwa ni kusambaza mipira kwa pasi fupi na za mbali zenye macho. 

Wakati Kocha Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ alishaithibitisha Mwanaspoti mapema alishasaini mkataba wa miaka miwili na ikamtambulisha kocha msaidizi, Patrick Mabedi, ishara Folz alikuwa hana muda mrefu Jangwani zilikuwa wazi.

Lakini kabla ya yote haya, kulikuwa kuna mambo matano ambayo Folz alikuwa anajifichia na kuupa mtihani uongozi wa Yanga kumfuta kazi Mfaransa huyo.

FOL 05

MATOKEO NA KOMBE JUU

Licha ya mashabiki wa Yanga kulalamika kwamba timu yao haichezi vizuri, lawama ambazo alikuwa akishushiwa Folz, timu ilishinda mechi zake nne kati ya tano za kimashindano kabla ya kupoteza mechi ya kwanza juzi huko Malawi.

Yanga ya Folz iliifunga Simba 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamiii na kuchukua taji hilo la kwanza msimu huu, kisha ikaitandika Wiliete ya Angola ugenini 3-0 kisha nyumbani 2-0 katika mechi mbili za hatua ya awali ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuichapa Pamba Jiji ya Mwanza 3-0 katioka ufunguzi wa Ligi Kuu Bara na mwisho ikatoa sare ugenini dhidi ya Mbeya Kwanza.

FOL 01

VIWANGO WAPINZANI

Hoja ya pili iliyombeba Folz ni ubora wa wapinzani. Ungeweza kusema mashabiki wa Yanga wanailinganisha timu yao na viwango vya wapinzani lakini bado unapata shaka kwa kuwa hakuna timu ambayo imechanganya na kuonyesha kiwango kikubwa.

Ukiitazama Simba unaikosa hoja hii kwamba wapinzani wa Yanga wanacheza vizuri, bado mambo hayajatulia kabisa kwa wekundu hao, ukihamia Azam nako mambo ni yaleyale ikiwa chini ya kocha mpya Florent Ibenge bado mambo hayajatulia ikiwa pia ndani ya mechi zake nne za mashindano yote imetoa sare moja na kushinda tatu.

Hapa tafsiri rahisi unayoipata ni bado ni mapema sana kwa timu zote kujadiliwa kwa hoja wachezaji au kocha hafai kutokana na msimu ndiyo kwanza una mechi mbili tu kwa timu zote kuanzia ndani na Kimataifa.

FOL 02

UKAMILIFU WA KIKOSI

Ukiangalia tangu Folz alipoanza kufanya kazi Yanga, hupati siku 15-20 ambazo amekaa na kikosi chake kizima mazoezini.

Yanga imekuwa na ratiba ya kujiandaa na msimu mpya kwa wachezaji wake kutokamilika kutokana na sababu ambazo zipo nje ya Folz na hata mabosi wa timu hiyo.

Kwenye mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya Folz amekuwa akipata nafasi ndogo sana ya kuwa na timu yake kamili, hatua ambayo kitaalam ni vigumu kwa kocha kufanya mambo yake kwa utulivu mkubwa.

Kuna wakati Folz alilazimika hadi kuchukua wachezaji wa timu za vijana kufanya nao mazoezi ili kuongeza idadi ya wachezaji kwenye kikosi cha kwanza.

FOL 03

WACHEZAJI TIMU ZA TAIFA

Wakati Folz anafika alikutana na ratiba ya uwepo wa Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN na Taifa Stars ilikuwa na wachezaji sita wa Yanga na kati ya hao watano walikuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza na mmoja akiwa benchi.

Wachezaji hao watano ni wale ambao pia wana sifa za kuingia kikosi cha kwanza cha Yanga wakiwemo mabeki Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Mohammed Hussein Tshabalala, Mudathir Yahaya na mshambuliaji Clement Mzize huku benchi akiwa Shekhan Khamis.

Baada ya Stars kutolewa robo fainali, ikafuata ratiba ya mechi za mtoano kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia na iliwazuia wachezaji hao kurudi klabuni kwao na hata sasa ligi imesimama tena kwa ratiba hiyohiyo.

Yanga kwenye ratiba ya mechi hizo za kalenda ya Fifa inaathirika zaidi kwa njia chanya kwa kupoteza kuanzia wachezaji 10 kwenda kujiunga na mataifa yao hatua ambayo ni wazi kwa kocha mpya anayejenga kikosi chake ni vigumu kutengeneza mambo kama ambavyo anakutana nayo Folz.

FOL 04

WACHEZAJI WAPYA, KOCHA MPYA

Soka ni sayansi kwa sasa wanachotaka mashabiki wa Yanga ni kuona soka la nguvu linapigwa lakini wanasahau sayansi hiyo inawazuia kuona mazuri hayo kwa haraka kiasi hicho kutokana na muda kutotosha.

Folz anahitaji muda kujenga timu yake, ni mapema kuonekana kama hatoshi kuiongoza timu hiyo, hasa wakati huu ambao msimu wa mashindano unaanza na yeye akiwa mpya kwenye timu mpya, anahitaji kuongezewa utulivu ili afanye kazi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *