
Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza tangu amuanike katika mitandao ya kijamii mke wake anayejulikana kwa jina la Hafsa Massudi, raia wa Burundi, msanii wa Bongo Fleva Ibraah, amefichua alivyompata mrembo huyo.
Ibraah ambaye kwasasa anatamba na wimbo wa ‘Beichee’ ameliambia Mwananchi kuwa amempata mke huyo mtandaoni baada ya kuachia wimbo wake wa ‘Tunapendana’ kwenye Insta Story yake ambako binti huyo alikuja ku-comment.
“Mimi nashangaa sana nilivyooa watu wengi walishangazwa eti wakawa wanajiuliza nimeoaje oaje, wengine wakasema imekuwa ndoa ya ghafla, kumbe walikuwa hawajui kama huyu mwanamke nilikuwa naye muda mrefu, sema mimi huwa sipendi mambo ya kuanika uhusiano wangu hadharani .
“Na jinsi nilivyompata ni kutokana na wimbo wangu wa ‘Tunapendana’ nilipoutoa niliuweka kwenye Insta Story yangu ya akaunti yangu ya Instagram, baada ya hapo yeye akaandika maoni yake ya kusifu kuwa ni kazi nzuri, nikamwambia asante, hapo ndio mambo mengine yakafuata hadi kufikia makubaliano ya kufunga ndoa,” amesema Ibraah.
Aidha, Ibraah ameeleza sababu ya kuishi tofauti na mke wake akisema inatokana na makubaliano yao kwani muda sio mrefu wanatarajia kupata mtoto.
“Kuishi tofauti na mke wangu sio sababu ya watu kusambaza habari za madai kuwa nimefunga ndoa feki, maana nimesikia hizi taarifa kuwa hakuna ndoa bali ni feki, sasa niwaambie tu watu kuwa nimeoa ukweli kabisa ile ni ndoa halali na hivi karibuni tunatarajia kupata mtoto.
“Tulioana nchini Burundi halafu yeye mke wangu akarudi kuishi Ubelgiji na hii ni kwa makubaliano ya mimi na yeye kwa sababu ni mjamzito, maana wakati wa kuoana mke wangu alikuwa tayari mjamzito,” amesema.
Ibraah ambaye kwa takribani miaka mitano alikuwa mwanamuziki wa lebo ya Konde Music Worldwide inayomilikiwa na msanii Harmonize, alifunga ndoa Julai 2025 na sherehe ilifanyika nchini Burundi.