
Jeshi la Israel
limesema litaanza tena utekelezaji wa usitishaji mapigano huko Gaza baada ya
kufanya mashambulizi ya anga siku ya Jumapili kujibu kile ilichokiita “ukiukaji wa wazi” wa Hamas wa makubaliano hayo.
Mashambulizi
yalianza kusini mwa Gaza baada ya jeshi la Israel kusema “magaidi
walifyatua kombora la kifaru na milio ya risasi” kuelekea kwa wanajeshi wake
huko Rafah na kuua wanajeshi wawili.
Hamas iinasema “haijui” mapigano yoyote katika eneo lililo chini ya udhibiti wa
Israel.
Kufikia jioni,
Israel ilisema imefikia malengo ya Hamas kote Gaza, huku vyanzo vya hospitali
vikisema watu 44 waliuawa.
Hamas inasema kuwa imejitolea kusitisha mapigano, na kuishutumu Israel kwa ukiukaji na kuonya mashambulizi hayo yanaweza “kusambaratisha makubaliano ya kusitisha mapigano”.
Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, ilianza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba, ambapo mapigano yalikomeshwa mara moja, kuondolewa kwa sehemu ya wanajeshi wa Israel kwenye mstari unaojulikana kama mstari wa manjano kaskazini, mashariki na kusini mwa Gaza, na kuongezeka kwa misaada.
Hamas imewaachilia mateka wote walio hai, kurejesha miili 12 kati ya 28 ya waliofariki.
Israel kwa upande wake iliwaachia huru wafungwa 250 wa Kipalestina katika jela zake na wafungwa 1,718 kutoka Gaza, na kurejesha miili 15 ya Wapalestina kama malipo ya kila mabaki ya mateka wa Israel.