Walinzi wa Pwani ya Italia wamewaokoa wahajiri 91 na kuopoa miili ya watu wengine wawili kutoka kwenye mashua iliyokuwa hatarini kupeperushwa kwenye pwani ya Kisiwa cha Lampedusa katika Bahari ya Mediterania.

Taarifa iliyotolewa na Kamandi ya Walinzi wa Pwani imesema operesheni ya uokoaji ilianza kutekelezwa baada ya ndege ya uchunguzi ya Frontex kugundua mashua hiyo umbali wa maili 16 (kilomita 29.6) kutoka Lampedusa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, boti mbili za doria zilitumwa kwenye eneo la tukio, na kufanikiwa kuwafikisha kwenye sehemu salama watu  91.

Kwa mujibu wa Kamandi ya Walinzi wa Pwani ya Italia, wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo ya uokozi miili ya wanaume wawili pia ilipatikana ndani ya boti, na kwamba manusura wote walipelekwa Lampedusa na kukabidhiwa kwa timu za madaktari kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia imetangaza kuwa, jumla ya wahamiaji 55,948 wamewasili nchini humo kwa njia ya bahari kati ya mwanzo wa mwaka huu wa 2025 hadi Oktoba 17, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na 55,010 waliosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Njia ya Kati ya Mediterania inayojumuisha Italia, Malta, Libya na Tunisia ingali ni mojawapo ya njia za baharini zinazotumika kufanyia safari hatarishi zaidi za kuelekea barani Ulaya.

Boti zilizojaa kupita kiasi, upungufu wa maji mwilini, kukosa hewa na moshi wa injini ni sababu zinazoendelea kugharimu maisha ya watu wengi kila mwaka huku wahamiaji wakijaribu kutumia njia hizo hatarishi kwa ajili ya kufika kwenye fukwe za Ulaya…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *