Unafahamu kuwa amejifunza siasa zaidi kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya baada ya uhuru.

Jaramogi Ajuma Oginga Odinga alizaliwa Oktoba 1911 na alihusika pakubwa katika harakati za kutetea uhuru wa Kenya. Awali alifahamika kama Obadiah Adonija lakini akajivua majina yaliyoonekana kunasibishwa na ukoloni na kuwa Oginga Odinga.

Alikuwa makamu wa rais wa Kenya kuanzia Disemba 1964 hadi April 1966. Alijiunga na chama cha KANU mwaka 1960 akiwa pamoja na mwanaharakati na mwanasiasa Tom Mboya.

Akiwa makamu wa rais alitofautiana na kiongozi wa nchi wakati huo kutokana na Odinga kuegemea mifumo tofauti ya siasa duniani.

Alijiuzulu nafasi hiyo 1966 na kuondoka kwenye chama cha KANU na kuunda chama cha KPU.

Mwaka 1969 alikamatwa baada ya yeye kutoleana maneno makali hadharani na rais Jomo Kenyatta, pamoja na watu 11 kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika vurugu magharibi mwa Kenya.

Alikuwa kizuizini kwa miezi 18 hadi alipoachiliwa huru pamoja na wengine mwaka 1971. Katika jaribio la kupindua serikali ya awamu ya pili ya Daniel arap  Moi 1982, Jaramogi Oginga Odinga aliwekwa chini ya ulinzi akiwa nyumbani.

Baada ya katiba kubadilishwa na mfumo wa chama kimoja kuondolewa aliunda chama cha upinzani pamoja na wengine cha FORD 1991.

Kabla ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1992, FORD iligawanyika mara mbili FORD Kenya na Ford Asili. Aligombea urais kwa tiketi ya chama cha FORD Kenya, lakini akamaliza nafasi ya nne na asilimia 17.5 ya kura.

Alifariki dunia Januari 1994 akiwa na umri wa miaka 82.

CHANZO:TRT Afrika Swahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *