Picha yenye mchanganyiko inayomwonyesha Emily, mwanamke mwenye nywele ndefu za kahawia, akiwa amepona, akitabasamu kwenye kioo huku akiwa amebandika plasta usoni na baada ya kupona kabisa bila kuvaa bandeji.

Chanzo cha picha, @hotgirlenhancements

    • Author, Ruth Clegg
    • Nafasi, Health and wellbeing reporter

Upasuaji wa kuvuta ngozi ya uso, maarufu kama facelift, sasa unaingia katika hatua mpya ya umaarufu.

Ukitazama kwa haraka mitandao ya kijamii, utakutana na maelfu ya machapisho kutoka kwa vijana wa miaka ya mwisho ya 20 hadi 30 wakijadili aina mbalimbali za upasuaji huu: mini facelift, ponytail facelift, na deep plane facelift.

Zamani, upasuaji huu ulionekana kuwa wa watu matajiri waliokomaa kiumri. Lakini hali imebadilika, idadi kubwa ya vijana wadogo sasa wanachagua kufanyiwa upasuaji huu kwa hiari.

Wengi hawasiti kushiriki picha zao kabla na baada ya upasuaji, pamoja na zile za kipindi cha kupona ambacho huwa cha uchungu na kujaa uvimbe mkubwa.

Huu si tena upasuaji unaofanywa kwa siri; watu mashuhuri kama Kris Jenner, Catt Sadler na Marc Jacobs wamezungumza waziwazi kuhusu safari zao za upasuaji. Wengine wengi wanaaminika kuwa wamewahi kufanyiwa.

Upasuaji wa kuvuta uso mara nyingi huonekana kama hatua ya mwisho kabisa ya urembo, aina kubwa na hatarishi zaidi ya upasuaji wa kubadili muonekano.

Lakini je, watu wamefikia hatua ya kutojiamini kiasi cha kuwa tayari kutumia maelfu ya paundi au dola kurekebisha sura zao ili kupendeza zaidi kwenye mitandao ya kijamii?

Au pengine, baada ya miaka ya kutumia njia zisizo za upasuaji kama Botox yaani sindano za kujazia ngozi, sasa kuvutwa kwa ngozi hadi mashavuni na kuhamishwa kwa tishu na mafuta ya usoni kunaonekana kuwa hatua inayofuata ya kawaida na yenye matokeo ya muda mrefu zaidi?

Emily baada ya upasuaji. Ana plasta kwenye paji la uso na mashavu na vilevile kwenye pua yake. Anainua vidole viwili kwenye kamera katika ishara ya v akiwa amelala kitandani

Chanzo cha picha, @hotgirlenhancements

Kwa Emily, aliyefanyiwa upasuaji huo akiwa na miaka 28, lengo lilikuwa kupata sura ya “kukakamaa” yaani taya iliyochongwa vyema, mashavu yaliyoinuka, na macho ya umbo la mbweha (fox eyes). Anasema upasuaji wake nchini Uturuki ulimbadilisha maisha kabisa, na hajutii hatua hiyo.

“Kwa ujumla, nilifanyiwa upasuaji sita kwa wakati mmoja,” anaeleza. “Ni pamoja na kuvutwa kwa sehemu ya katikati ya uso, kuinuliwa kwa mdomo, na upasuaji wa pua.”

Emily, mfanyabiashara kutoka Toronto, Kanada, anaeleza kuwa daktari wake wa upasuaji alimpigia wimbo wake anaoupenda wakati akiwekwa usingizi wa ganzi ya jumla. “Nililala, nikaamka nikiwa natapika, nikiwa na uso na pua mpya.”

Mchakato wa kupona haukuwa mwepesi. Maumivu na uvimbe vilianza kupungua baada ya wiki chache, lakini ilimchukua miezi sita kurejesha hisia katika baadhi ya sehemu za mashavu yake.

Je, angefanya tena? Anasita kabla ya kujibu.

“Tangu nifanyiwe upasuaji, maisha yangu yamebadilika. Sasa ninaishi kwa afya zaidi, nakunywa pombe kidogo, najali ngozi yangu, nalala vizuri. Pengine kama ningejua haya yote kabla, nisingefanya upasuaji huu.”

“Hata mama yangu hakujua mpaka nilipomwambia siku chache baada ya upasuaji.”

Anatafakari kwa muda, kisha anasema:

“Lakini nilitaka kuwa toleo bora la mimi mwenyewe na sasa naamini nimefikia hapo.”

Pia unaweza kusoma:

Takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Urembo nchini Uingereza (BAAPS) zinaonyesha ongezeko la asilimia 8 la upasuaji wa kuvuta uso katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Ingawa takwimu hizo hazibainishi umri wa wagonjwa, wanachama wengi wa chama hicho wanasema kwamba kundi la watu linalofanyiwa upasuaji huu linazidi kubadilika likiwa na vijana zaidi.

Mwelekeo huu unaonekana pia sehemu nyingine za dunia. Katika Marekani, Shirika la Madaktari wa Upasuaji wa Urembo linaona ongezeko la watu wa kizazi cha Gen X (miaka 45–60) wanaochagua njia hii ya kurekebisha muonekano wa uso.

Daktari Nora Nugent, rais wa BAAPS, anasema mabadiliko haya yanasababishwa na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni matumizi ya dawa za kupunguza uzito.

“Kupungua uzito kwa haraka kupitia dawa hizi kunaweza kuacha ngozi iliyolegea. Upasuaji wa kuvuta ngozi husaidia kurejesha umbo la uso,” anasema. “Mbinu za upasuaji zimeboreshwa sana siku hizi hatuoni tena matokeo ya uso unaovutwa kupita kiasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.”

Mchoro unaoonyesha jinsi kiinua uso kinafanywa. Kuna picha mbili za uso na shingo na sehemu za msalaba zinazoonyesha chini ya ngozi Mchoro huu unaonyesha jinsi madaktari wa upasuaji wanavyokata chini ya tabaka kadhaa kabla ya kufikia ndege ya kina ambayo wanaunda upya

Chanzo cha picha, BAAPS

Hata hivyo, anaonya kuwa bado huu ni upasuaji mkubwa unaopaswa kufanywa tu na daktari aliyebobea katika upasuaji wa urembo, ndani ya kituo kilichosajiliwa na chenye vifaa kamili.

Katika kliniki yake huko Bristol, daktari bingwa wa upasuaji Simon Lee ameendesha mamia ya upasuaji wa kuvuta uso. Anaonyesha video ya mchakato huo, ambapo mgonjwa huwa macho wakati wote, akiwa amedungwa ganzi ya sehemu ndogo.

Katika video hiyo, daktari anafanya michanjo midogo usoni kabla ya kuingia ndani ya ngozi, mafuta na tabaka la misuli linalohusiana na sura ya uso (SMAS), kisha kufikia sehemu ya ndani zaidi ya uso ambako hupanga upya tishu na misuli ili kuunda sura mpya.

Baada ya saa nne za upasuaji, mgonjwa anatoa tabasamu la faraja.

Kwa mujibu wa daktari Lee, sehemu ya mvuto wa upasuaji huu ni urahisi wake wa kisasa.

Zamani ilihitaji chumba cha upasuaji hospitalini na ganzi ya kulala, lakini sasa anaweza kufanya upasuaji wa uso na shingo bila kulaza mgonjwa.

Anasema sekta hii ipo katika kipindi cha maendeleo ya kasi.

Mbali na upasuaji wa kawaida unaolenga taya na shingo, sasa kuna mbinu mpya zinazolenga sehemu za juu za uso ambapo mabadiliko ya uzee huanza kuonekana mapema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa upasuaji huu unawafaa zaidi walio na umri wa zaidi ya miaka 40.

Kwa watu wa miaka 20 au 30, ni nadra sana kufanya upasuaji wa aina hii, kwani ni mgumu na unahusisha hatari mbalimbali.

Baadhi ya hatari hizo ni pamoja na kutokea kwa damu kujikusanya chini ya ngozi (hematoma), maambukizi, kuumia kwa neva, na hata kupoteza nywele sehemu ya kichwa.

Gharama ya “facelift” au kuunga uso nchini Uingereza ni kati ya £15,000 hadi £45,000, lakini baadhi ya kliniki hutoa huduma hiyo kwa kiasi cha chini hadi £5,000. Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kufanya utafiti wa kina kabla ya kuchagua daktari.

Mchanganyiko wa Julia kabla na baada ya upasuaji. Katika picha iliyotangulia anatazama kamera na amevaa hereni za nyota ya fedha na mkufu wa cheni ya fedha. Katika picha ya kati ana plasta usoni na baadhi ya alama za kalamu bado zinaweza kuonekana. Macho yake yamevimba na ya rangi ya zambarau. Picha ya tatu inamuonyesha akiwa hana bandeji wala plasta. Nywele zake ndefu nyeusi zinaning'inia upande wowote wa uso wake.

Chanzo cha picha, Julia Gilando

Julia Gilando, mwenye umri wa miaka 34, aliamua kufanyiwa “facelift” yaani kuunda wajihi baada ya kuwa na tatizo la kutolingana kwa pande za uso kutokana na matatizo ya taya aliyoyapata awali.

Licha ya marafiki zake kumwambia kwamba hawaoni tatizo lolote, Julia aliamini hisia zake na alisafiri hadi Uturuki kwa upasuaji huo, uliomgharimu dola 8,000 (£6,000).

Ingawa wapo wanaoonya kuhusu hatari za kufanyiwa upasuaji wa urembo nje ya nchi, Uturuki imeendelea kuvutia wateja wengi kutokana na bei nafuu.

“Mwanzoni nilihisi kama ni wazo la kipuuzi,” anasema Julia, mtaalamu wa afya. “Lakini nilifanya utafiti wangu, nikajiamini, na nikaenda. Ingawa nilikuwa peke yangu, nchi ya kigeni, na sikujua lugha, nilijikaza.”

“Baada ya upasuaji nilikaa hospitalini kwa siku mbili, kisha nikajitunza mwenyewe. Nilivimba hadi sikuweza kuona. Kulikuwa na vipindi vya huzuni, mabadiliko ya hisia yalikuwa makali sana.”

Watafiti wanaendelea kujiuliza kama kweli upasuaji wa urembo huongeza hali ya mtu kujithamini na kujiamini kama inavyodaiwa na sekta hiyo.

“Kuna shinikizo kubwa sana kwa sasa,” anasema Dk. Kirsty Garbett, mtafiti wa masuala ya sura kutoka Chuo Kikuu cha West England. “Haswa kwa upande wa uso tunajiona mara kwa mara kwenye video, mitandao ya kijamii, na kujilinganisha na wengine ni rahisi mno.”

Anaongeza kuwa kile tunachokiona mtandaoni si kila mara kinaakisi uhalisia.

“Teknolojia kama akili bandia (AI), pamoja na vichujio (filters), vinachangia sana kuunda ulimwengu wa uongo mtandaoni. Wakati huo huo, tunashuhudia ongezeko la hali ya kawaida ya watu kuona upasuaji wa urembo kama jambo la kawaida.”

Kwa upande mmoja, anasema watu maarufu kuzungumzia waziwazi kuhusu kufanyiwa kwao upasuaji kunaweza kusaidia kuvunja unyanyapaa. Lakini kwa upande mwingine, inahatarisha kuufanya upasuaji huo uonekane kama sehemu ya kawaida ya maisha jambo analoliona kuwa la kutia wasiwasi.

Mchanganyiko wa Caroline Stanbury upasuaji wa kabla na baada ya kuinua uso. Katika picha ya kwanza anatazama kamera akiwa na nywele zake za kimanjano zilizotengenezwa kwa mtindo wa kupeperushwa upande wake wa kulia. Amevaa fulana nyekundu na amevaa hereni kubwa za dhahabu na rangi ya mdomo nyekundu. Picha ya kati anaonekana akiwa amejifunga bandeji kichwani na amevaa gauni linaloonekana kuwa la hospitali. Katika picha ya tatu ana nywele ndefu za kuchekesha na amevaa juu ya kijani kibichi na mkufu wa lulu.

Chanzo cha picha, Caroline Stanbury

Caroline Stanbury, mtangazaji wa televisheni na mmoja wa waigizaji wa kipindi cha The Real Housewives of Dubai, alifanyiwa upasuaji wa kuvuta ngozi ya uso miaka miwili iliyopita akiwa na umri wa miaka 47 licha ya marafiki wengi kumwambia ni mapema mno kufanya hivyo.

“Ni jambo bora zaidi kuwahi kulifanyia mwili wangu,” anasema Caroline. “Sioni sababu ya kungoja hadi nifikie miaka ya 60 na kuwa na uhitaji mkubwa. Nataka kuonekana na kujihisi mzuri sasa.”

Baada ya miaka 20 ya kutumia Botox yaani dawa ya sindano ya kupumzisha misuli na sindano za kujazia, Caroline alihisi sura yake inaanza kubadilika isivyopendeza. Alilipa dola 45,000 (£34,000) kufanyiwa deep plane facelift (kuinua uso kwa kina) nchini Marekani.

“Bado naonekana kama mimi, lakini upasuaji huu umenipa miaka mingine 20 ya kujihisi vizuri,” anasema.

Lakini si kila daktari anayeunga mkono ongezeko hili la vijana kujitokeza kwa ajili ya upasuaji wa kuvuta ngozi ya uso.

Dkt. Alexis Verpaele, daktari bingwa wa upasuaji wa urembo kutoka Ubelgiji anayehudumia wateja kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Uingereza, anasema ana wasiwasi kuhusu idadi inayoongezeka ya vijana wanaokuja kwa ajili ya matibabu haya.

Anasema mara nyingi huwa anazungumza nao kwa kina ili kueleza mbinu mbadala ambazo zinaweza kufanikisha matokeo yanayofanana bila kupitia upasuaji mkubwa.

“Ukifanya facelift(kuunda wajihi) ukiwa na miaka 20 na zaidi, na tukijua kwamba inaweza kudumu kwa miaka 10 hadi 15,” anasema,

“Basi kufikia miaka 60, huenda utakuwa umefanyiwa facelift tatu,” anasema De Verpaele.

Lakini ukweli ni kwamba uso ni sehemu nyeti sana ya mwili. Kuufanyia upasuaji mkubwa mara kwa mara ni mateso makubwa kwa ngozi na tishu zake,” anaendelea.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *