
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, miundomsingi ya makombora na ulinzi imebaki imara kama ilivyokuwa kabla ya Vita vya Siku 12 na kubainisha kwa kusema: “mkwaruzo wenye ukubwa hata wa ubawa wa nzi” haukufanywa kwenye makombora ya Iran.
Akizungumza katika mahojiano, Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi, ambaye alikuwa Naibu Mratibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wakati wa Vita vya Siku 12, amebainisha kwa kina mwenendo wa matukio ya kijeshi yaliyojiri na athari za uvamizi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel katika vita hivyo na kusisitiza kuwa kikosi cha makombora cha Iran kiliibuka salama bila ya kuathirika.
“Hakuna hata mkwaruzo, wala mstari mwembamba wenye ukubwa wa ubawa wa nzi, ambao umefanywa kwenye mfumo mkuu wa makombora yetu,” ameeleza Jenerali Naqdi na kuongeza kuwa hakuna wowote katika “miji ya makombora” ya Iran ulioharibiwa na kwamba shughuli za urushaji makombora zilianza tena haraka baada ya mashambulizi.
Katika mahojiano hayo, Naibu Mratibu wa IRGC katika Vita vya Siku 12 amebainisha pia kwamba, wakati wa uvamizi huo wa utawala wa kizayuni ilidhihirika wazi kuwa Iran haikuwa inakabiliana na Israeli pekee, bali ilikuwa inapigana vita na muungano mpana zaidi.
“Tuko kwenye makabaliano na NATO; kuna Marekani, Uingereza, Ufaransa, Jordan na utawala wa Kizayuni,” ameeleza Jenerali Naqdi.
Kamanda huyo wa IRGC ameashiria vituo vya Marekani vilivyoko katika nchi jirani, rada, vifaa vya kusikilizia, balozi za kigeni zilizoko mjini Tehran, pamoja na satalaiti, na kueleza kwamba, zote hizo zinatoa taarifa kwa Israel za kila kinachojiri kwa wakati.
Aidha, amesema makumi ya ndege zisizo na rubani za kigeni huwa zinapiga doria kila siku katika Ghuba ya Uajemi, zikichunguza hadi ndani kabisa ya ardhi ya Iran.
Mnamo Juni 13, utawala wa kizayuni wa Israel ulianzisha uchokozi usio na sababu dhidi ya Iran, na kusababisha vita vya siku 12 vilivyoua karibu watu 1,064 hapa nchini, wakiwemo makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.
Marekani pia iliingia vitani kuusaidia utawala wa kizayuni kwa kushambulia kwa mabomu maeneo matatu ya vituo vya nyuklia vya Iran katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Hata hivyo, operesheni kali za kulipiza kisasi zilizotekelezwa kwa mafanikio na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, zipelekea kusimamishwa uvamizi wa kigaidi ulioanzishwa na Israel na Marekani mnamo tarehe 24 Juni…/