
Chanzo cha picha, EPL
Mwishoni mwa wiki hii, mashabiki wa Ligi Kuu ya England walishuhudia matukio ya kipekee: rekodi kuvunjwa, historia kuandikwa upya na ‘laana’ kutoweka na ubabe mpya kujitokeza katika klabu kubwa na ndogo.
Kutoka Anfield hadi Etihad, wikiendi hii imeacha alama ya kudumu katika kumbukumbu za mashabiki wa soka duniani kote.
Kabla ya kukwambia kilichotokea, nakukumbusha Arsenal inayoongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa alama tatu, iliichapa Fulham ugenini bao 1-0, Man City iliichapa Everton 2-0.
Kwa upande wa Chelsea iliilaza Nottigham Forest 3-0 ugenini na Manchester United ikaushangaza ulimwengu kwa kuichapa Liverpool 2-1 katika uwanja mgumu wa ugenini wa Anfield.
Manchester United yavunja laana ya Anfield baada ya miaka 10
Klabu ya Manchester United imepamba vichwa vya habari baada ya kushinda 2–1 dhidi ya Liverpool kwenye uwanja wa Anfield, ushindi wao wa kwanza katika ardhi hiyo tangu Januari 2016. Bao la ushindi lililowekwa wavuni kwa kichwa na mlinzi Harry Maguire dakika za mwisho lilihakikisha historia mpya, likiifuta miaka kumi ya ‘laana’ kwa mashabiki wa United katika uwanja ambao ulikuwa mgumu zaidi kwao.
Ushindi huo pia ulikuwa wa kipekee kwa kocha mpya Rúben Amorim, kwani uliashiria mara ya kwanza kwa Manchester United kushinda mechi mbili mfululizo za ligi tangu ajiunge mwezi Novemba 2024. Tangu afike Old Trafford, Amorim amekuwa akijaribu kuibadilisha United iwe timu yenye nidhamu na umakini wa kiufundi, na matokeo haya yanaonekana kuashiria mwanzo wa mabadiliko hayo.
Kwa upande mwingine, Liverpool imejikuta ikivunja rekodi mbaya, ambapo klabu hiyo imepoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014. Kipigo cha Anfield kimeongeza shinikizo kwa kocha Arne Slot, ambaye anakabiliwa na changamoto ya kurejesha ari ya timu ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa na ubabe mkubwa nyumbani na barani Ulaya.
Haaland, City na ubabe wa mabao

Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester City yaendeleza ubabe wake katika uwanja wake wa nyumbani wa Etihad ikiishinda Everton maba0 2-0. Erling Haaland aliendelea kuwa tishio baada ya kufunga mabao mawili, na kufikisha mabao 11 katika mechi 8 za kwanza za ligi msimu huu, akionesha dalili za kuvunja tena rekodi yake binafsi ya mabao 36 kwa msimu.
Mshambuliaji huyo Mnorway kwa sasa anaongoza kwa mbio za kufumania mabao, akimuacha Antoine Semenyo kwa mabao 5, ambaye hakufunga katika mchezo wa sare ya 3-3 timu yake ya AFC Bournemouth ilipokutana na Crystal Palace.
Mchezo huo wa Bournemouth dhidi ya Palace unatajwa pia kuingia katika rekodi ya michezo bora ya ligi kuu kwa msimu huu. Mechi hiyo ilikuwa ya kustaajabisha: mshambuliaji chipukizi Eli Kroupi alijitangaza katika Ligi kuu kwa kufunga mabao mawili, akicheza mechi yake ya kwanza ya ligi. Bournemouth waliongoza 2–0 mpaka mapumziko kupitia mabao hayo, kabla ya Crystal Palace kujibu mapigo kwa mabao mawili ndani ya dakika tano kupitia Jean-Philippe Mateta.
Hata hivyo, ‘drama’ haikuishia hapo: Ryan Christie aliyejaribu kuipa Bournemouth ushindi akifunga bao la tatu dakika ya 89, lakini Mateta akafunga balo la tatu ‘hat-trick’ kwenye muda wa nyongeza. Mechi ilimalizika kwa sare, huku matukio haya yote yakionyesha kiwango cha juu cha ushindani kwenye ligi msimu huu.
Chelsea yampa Ange rekodi ya ukocha ya muda mfupi ‘siku 39’

Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea ilirejea kwenye ubora wake baada ya kupata ushindi wa 3–0 dhidi ya Nottingham Forest ugenini, kwenye uwanja wa City Ground. Matokeo hayo yaliweka rekodi ndogo muhimu kwa klabu hiyo, ni mara ya kwanza tangu Machi 2023 kwa Chelsea kushinda mechi tatu mfululizo za ligi bila kuruhusu bao.
Katika mechi hiyo, Josh Acheampong alifunga bao la kwanza, ambalo ni la kwanza kwake kwenye EPL, akifunga kwa kichwa baada ya krosi nzuri kutoka upande wa kushoto. Bao la pili lilifungwa na Pedro Neto, ambaye alimalizia pasi nzuri kutoka kwa Reece James. James mwenyewe alifunga bao la tatu kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Forest.
Baada ya kipigo hicho, klabu ya Nottingham Forest ilitangaza kumtimua kazi kocha Ange Postecoglou aliyekuwa ameiongoza timu hiyo kwa siku 39 pekee tangu kuteuliwa mwezi Septemba. Kufukuzwa kwake kumeweka rekodi ya kipekee: ni mmoja wa makocha wa kudumu waliodumu kwa muda mfupi zaidi katika historia ya EPL.
Takwimu zinaonyesha kuwa Postecoglou hakushinda mechi yoyote kati ya mechi nane alizoiongoza Forest katika mashindano yote, hali iliyoiweka klabu hiyo karibu na eneo la kushuka daraja. Kwa klabu yenye historia ndefu kama Nottingham Forest, kutoshinda mechi nane mfululizo katika mwanzo wa msimu ni mwendelezo mbaya zaidi tangu msimu wa 1992/93, waliposhuka daraja kwa mara ya kwanza.