
Umoja wa Afrika (AU) ulisimamisha uanachama wa Madagascar kufuatia mapinduzi ya kumuondoa madarakani Rais Andry Rajoelina, yaliyokuja baada ya wiki tatu za maandamano ya kuipinga serikali yaliyoongozwa na vijana almaarufu Gen Z.
Madagascar sasa ni miongoni mwa nchi nyingine sita ambazo uanachama wake ulisimamishwa na Umoja huo kati ya mwaka 2019 na 2023. Sudan, Mali, Guinea, Burkina Faso, Niger na Gabon, zote hizo kutokana na mapinduzi ya kijeshi na mabadiliko ya serikali yanayochukuliwa na Umoja huo wa Afrika kuwa kinyume na katiba.
Katika taarifa baada ya mkutano wake wa dharura wa Baraza la Amani na Usalama kuhusu Madagascar, mwenyekiti wa AU Mahmoud Ali Youssouf alibainisha kuwa, utawala wa sheria lazima uwe juu ya utawala wa nguvu na kuhalalisha kusimamishwa huko kwa Madagascarkwa msingi wa sheria na majadiliano.
Hatua hiyo imezua shutuma kutoka kwa wachambuzi kama vile Fidel Amakye Owusu, mchambuzi wa masuala ya usalama aliyebobea katika masuala ya Afrika na siasa za kijiografia, ambaye anasema itifaki ya Umoja wa Afrika inayodhibiti matukio yanayohusiana na mapinduzi barani Afrika ni ya mwitikio zaidi.
Ryan Cummings, mkurugenzi wa uchambuzi katika kampuni ya kudhibiti hatari inayolenga Afrika ya Signal Risk, anaamini kuwa kusimamishwa uanachama wa AU kumekuwa njia pekee ya jumuiya hiyo ya kushughulikia vitendo visivyo vya kidemokrasia.
Hatua za AU hazizui mabadiliko mabaya ya serikali yanayofanyika Afrika
Ameiambia DW kwamba anafikiri kusimamishwa kwa uanachama wa Madagascar katika Umoja wa Afrika kutokana na mapinduzi yaliofanyika kunadhihirisha taratibu finyu ambazo Umoja huo wa Afrika uko nazo kuhakikisha kuwa kuna aina fulani ya uwajibikaji au athari.
Kulingana na Cummings, AU inasimamisha uanachama wa mataifa ili kuonyesha kutoridhika kwake na mabadiliko ya mamlaka kinyume na katiba miongoni mwa nchi wanachama kinyume na katiba.
Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS) pia inaona kusimamishwa uanachama wa AU kama njia ya kubadilisha mienendo ya nchi wanachama wanaokiuka sheria na kukuza kanuni za pamoja. Hata hivyo, katika hali nyingi, hatua za Umoja huo hazizui mabadiliko ya serikali kinyume na katiba.
Ripoti ya ISS ya mwaka 2023, ilisema vikwazo vilivyotekelezwa dhidi ya Sudan, Mali, na Burkina Faso havijazuia kurudiwa kwa mapinduzi katika maeneo hayo wala hayajazuia mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea, Niger, Chad na Gabon. Licha ya hatua hizi kali, nchi kadhaa bado hazijarejesha utulivu wa kikatiba au kurejesha utawala wa kidemokrasia.
AU ilianzisha Chombo cha Utatuzi wa Migogoro, Amani na Usalama ili kutoa hatua madhubuti za kuzuia kuongezeka kwa migogoro ya ndani ya nchi wanachama.
Kulingana na Umoja wa Afrika, chombo hicho cha kufanya maamuzi ni mpango wa pamoja wa usalama na onyo la mapema linalokusudiwa kuwezesha majibu ya haraka na ufanisi kwa mizozo na hali ya mgogoro barani Afrika. Hata hivyo, wakosoaji wanasema chombo hicho huchelewesha kutekeleza hatua hiyo.