Mamilioni ya Wamarekani waliingia mitaani katika maandamano ya nchi nzima wakiimba “No Kings” kupinga muhula wa pili wa rais Donald Trump na kile wanachokiita “mienendo yake ya kimabavu.”
Maandamano ya kitaifa ya “Hapana kwa Wafalme” yalifanyika Oktoba 18, 2025, katika majimbo yote 50 nchini Marekani na katika baadhi ya nchi nyingine, kama vile Kanada, Mexico, na nchi kadhaa za Ulaya. Tukio hilo, wimbi la pili kubwa la maandamano dhidi ya muhula wa pili wa Donald Trump, liliandaliwa na mtandao wa mashirika zaidi ya 200 yanayoendelea, pamoja na Indivisible, MoveOn, Human Rights Watch na vyama vya wafanyikazi.
Kwa makadirio watu milioni 4 hadi 6 walishiriki maandamano hayo. Maandamano hayo yalielezwa kuwa makubwa zaidi kufanyika siku moja katika historia ya hivi karibuni ya Marekani, yakipiku maandamano ya 2017 dhidi ya Trump.
Maandamano hayo yalikuwa na malengo kadhaa; kauli mbiu ya “No Kings” inarejelea moja kwa moja kwa vitendo na matamshi ya Donald Trump, ambayo waandamanaji wanaona kuwa ni jaribio la kudhoofisha demokrasia na kuanzisha mfumo wa kimabavu nchini Marekani.
Waandamanaji wanaamini kuwa, maneno ya Trump kuhusu kutaka “mamlaka ya kudumu” au kujaribu kukwepa mipaka ya kisheria kama vile muhula wa tatu wa urais, yanatishia sana Katiba.

Maandamano hayo sambamba na kusisitiza kwamba, Marekani haina mfalme yamefanyika kwa lengo la kurejesha imani lwa misingi ya kidemokrasia.
Mojawapo ya msukumo mkuu ilikuwa radiamali kwa sera kali za utawala za uhamiaji, hasa operesheni kubwa za Vikosi vya Uhamiaji (ICE) katika miji inayodhibitiwa na Wademokrats. Waandamanaji waliona oparesheni hizi kama shambulio kwa jamii na matumizi haramu ya jeshi kukandamiza maandamano na kudhibiti miji bila kibali cha eneo husika, wakilaani kama uvamizi wa kijeshi na wakitaka kukomeshwa.
Waandamanaji pia walipinga kupunguzwa kwa huduma za umma kama vile afya na elimu na sera za kiuchumi ambazo zinapendelea mabilionea kama vile Elon Musk, Jeff Bezos na Mark Zuckerberg.
Seneta Bernie Sanders amezitaja sera hizi kuwa uchumi rafiki kwa mabilionea na akatoa wito wa ugawaji upya wa haki wa rasilimali.
Shutuma za ufisadi wa kifedha na matumizi ya pesa za ushuru kwa masilahi ya binafsi ya Trump pia zilikosolewa katika maandamano haya ya kitaifa nchini Marekani.
Lengo la muda mrefu la maandamano hayo lilikuwa kuunda wingi wa upinzani wa kimyakimya dhidi ya Trump, kupinga madai yake ya kuungwa mkono na wananchi wengi. Waandaaji walibuni maandamano hayo kama chachu ya vuguvugu pana linalolenga kuhamasisha watu kwa ajili ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2026. Maandamano yamekuwa na matokeo muhimu ya awali na yanaweza kuwa na athari kubwa.

Maandamano hayo, ambayo yalivuta hisia za kimataifa na watu mashuhuri kama vile Bernie Sanders, John Cusack, Robert De Niro na Bill Nye, yalivutia mamilioni ya watu, wakiwemo vijana, maveterani na jamii za walio wachache, wakionyesha umoja wenye wigo mpana dhidi ya sera za Trump.
Wademokrats kama vile Chuck Schumer na Cory Booker waliyaita maandamano hayo kuwa ni onyesho la upendo kwa Marekani, wakati Republican kama Mike Johnson na J.D. Vance walisema ni onyesho la chuki dhidi ya Marekani. Trump mwenyewe alikejeli maandamano hayo kwa kusambaza video ya kichekesho akiwadondoshea matope waandamanaji kutoka kwenye ndege ya kivita. Radiamali hizi zimedhihirisha kuweko mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani.
Wakati huo huo, maandamano hayo yamevuta hisia za kimataifa katika masuala ya demokrasia, uhamiaji, na haki za kiraia, na yameongeza mashinikizo kwa serikali kufikiria upya kutuma wanajeshi wa shirikisho mijini. Aidha maandamano hayo yanaweza kuimarisha kwa vuguvugu la upinzani wa raia na kuwa na taathira kwa uchaguzi wa 2026.

Hata hivyo, inaonekana kuwa hata maandamano hayo hayawezi kumfanya Trump na wafuasi wake kutafakari upya mipango yao. Warepublican, hususan vuguvugu la “Make America Great Again” (MAGA) linalomuunga mkono Trump, wanahisi kuwa wana fursa ya kihistoria ya kutekeleza ajenda za kihafidhina nchini Marekani na kuwatenga waliberali na wafuasi wa mrengo wa kushoto kutoka nyanja ya umma. Kwa muktadha huo, inatarajiwa kwamba mivutano ya kisiasa na kijamii nchini Marekani itaongezeka na kushadidi katika wiki na miezi ijayo.