Makundi mbalimbali yanayohusishwa na Al-Qaeda hasa kundi maarufu la Group for the Support of Islam and Muslims (JNIM) pamoja na lile la Dola la Kiislamu (IS), sasa yanashambulia karibu maeneo yote ya Mali na Burkina Faso, kutoka magharibi mwa Niger na Nigeria hadi mipakani mwa Senegal.
Haya ni kwa mujibu wa utafiti wa shirika la habari la AFP wa miaka sita kuhusu operesheni zilizorekodiwa na shirika huru linalofuatilia waathirika wa migogoro duniani (ACLED).
Charlie Werb, mchambuzi kutoka taasisi ya Aldebaran Threat Consultants, alionya kwamba mgogoro wa kiusalama katika eneo la Sahel ni tata na hauna suluhisho la haraka.
Mashambulizi yanakaribia 30,000
Idadi ya mashambulizi ilipanda kutoka 1,900 mwaka 2019, yaliyokuwa yamejikita zaidi mpakani mwa Mali na Burkina Faso, hadi zaidi ya 5,500 mwaka 2024.
Tayari mashambulizi 3,800 yameripotiwa mwaka 2025 hadi Oktoba 10, na kufanya jumla ya mashambulizi kufikia 28,715 ndani ya kipindi cha takriban miaka sita.
Upanuzi wa Al-Qaeda hadi magharibi mwa Mali na kusini mwa Burkina Faso, na wa Dola la Kiislamu hadi magharibi mwa Niger na Nigeria, unamaanisha kuwa makundi ya kijihadi sasa yanafanya operesheni katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita milioni moja za mraba — mara mbili ya ukubwa wa Hispania.
Kiini kingine cha machafuko kipo karibu na Ziwa Chad, mashariki mwa Nigeria, ambako Boko Haram na tawi la Dola la Kiislamu la Afrika Magharibi (ISWAP) yanaendesha shughuli zake.
Ongezeko la idadi ya wapiganaji
Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, Al-Qaeda na Dola la Kiislamu wana jumla ya wapiganaji 7,000 hadi 9,000, huku ISWAP ikikadiriwa kuwa na 8,000 hadi 12,000.
Vifo vingi vimeripotiwa wakati wa mapigano na majeshi ya serikali, huku takriban watu 16,000 wakifariki katika mashambulizi dhidi ya raia. Zaidi ya watu 20,000 wameuawa nchini Nigeria, lakini Mali na Burkina Faso ndizo zimeathirika zaidi, zikichangia asilimia 56 ya vifo vya ukanda huo.
Zikiwa chini ya utawala wa kijeshi, nchi hizi mbili zimefukuza majeshi ya Magharibi hasa vikosi vya Ufaransa katika miaka ya karibuni. Mikakati yao imejikita katika nguvu za kijeshi, lakini, anasema Werb, matokeo yake “hayajawa bora, na katika hali mbaya zaidi, yameleta athari hasi.”
Mamlaka za kijeshi zinaonekana kushindwa kudhibiti kuongezeka kwa ushawishi wa wapiganaji wa Jihadi, hasa kutokana na kutojikita kushughulikia sababu za kijamii na kiuchumi za ukosefu wa usalama.
Tangu mwaka 2019, tawi la Al-Qaeda katika Sahel limepanua mashambulizi kutoka kaskazini mwa Burkina Faso na sasa limeizunguka Ouagadougou, likitishia mawasiliano na nchi jirani za Ivory Coast, Togo na Mali.