Dar es Salaam. Wakati Alice Haule akirejeshewa hati ya nyumba yake leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, baada ya kumalizika kwa mgogoro uliokuwa ukimkabili na mfanyabiashara Mohamed Yusufali, taarifa mpya zimeibuka kuhusu sakata hilo.

Alice, mjane aliyeondolewa na mabaunsa kwenye nyumba yake na vitu vya wapangaji kutupwa nje Septemba 23, 2025, kwa madai ni mvamizi kutokana na deni la marehemu mumewe, Justice Rugaibula.

Video za tukio hilo zilionesha mabaunsa waliodaiwa kutumwa na Yusufali wakimbeba juu juu Alice na kumtoa nje ya nyumba yake, huku vitu vya wapangaji wake, raia wa China vikitupwa nje kwa madai kuwa ni mvamizi.

Katika sakata hilo, Alice alidai kuwa nyumba hiyo waliinunua na marehemu mumewe mwaka 2008, na baadaye mumewe alikopeshana fedha Sh150 milioni na Yusufali, ambaye sasa anadai mumewe alimuuzia nyumba hiyo, jambo alilodai halina ukweli.

Mjane Alice alivyorejeshewa nyumba yake

Baada ya sakata hilo, Alice alifungua kesi ya madai namba 24541/2025 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, kutafuta haki yake.

Wakati kesi hiyo ikiitwa tena Oktoba 28, leo Oktoba 20, 2025, mjane huyo amekabidhiwa hati ya nyumba hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, baada ya uchunguzi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu mgogoro wa umiliki wa kiwanja namba 189 kilichopo eneo la Msasani Beach, jijini Dar es Salaam, kukamilika.

Hata hivyo, mapya yameibuka katika sakata hilo baada ya wakili Mpwaga Bernard, anayemwakilisha Yusufali, kueleza kwamba kilichotokea kwa mkuu wa mkoa hakihusiani na kesi iliyopo mahakamani.

“Kesi inakuja Oktoba 28, 2025, kulikuwa na amri za kimahakama za kutakiwa kuwasilisha utetezi, bado shtaka hili lipo mahakamani. Ukiachilia mbali mdai, wengine walikuwa na tarehe husika za kuwasilisha utetezi wao mahakamani, ikiwamo Msajili wa Ardhi, Kamishna wa Ardhi pamoja na mdaiwa wa kwanza ambaye ni mteja wangu (Yusufali),” amesema wakili huyo.

Wakati wakili wa Yusufali akisema hayo, wakili wa mjane huyo, Mwesigwa Mhingo, amesema kwa kuwa walichokuwa wakikitafuta mahakamani ni hati yao, kesi waliyoifungua dhidi ya Yusufali watakwenda kuifuta itakapotajwa Oktoba 28.

“Mahakamani kesi ipo, imepangwa Oktoba 28. Sisi tutakwenda kuomba kuiondoa kwa kuwa haina sababu tena,” amesema Mhingo.

Alichokisema Alice

Akizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya kukabidhiwa hati yake leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, Alice amesema kilichotokea ni mkono wa Mungu.

“Jambo hili limeenda miaka karibu 13, na miaka yote hiyo nilikuwa napambana. Huu ni wakati wa Mungu, nimepata haki yangu, nashukuru sana,” amesema Alice.

Amesema alipokea taarifa ya wito wa suala hilo saa 6 kasoro usiku wa kuamkia leo Jumatatu.

“Tulikuwa tumemaliza maombi ya familia, nikakuta missed call. Nikapiga simu haikupokelewa, baada ya dakika chache nikapigiwa, nikaambiwa, ‘Alice kesho saa 3 asubuhi tukutane ofisini kwa mkuu wa mkoa.’ Nikashtuka, nikasema sijui kuna nini.”

“Sikupata usingizi hadi alfajiri saa 11 nikajiandaa, nikatoka nyumbani. Saa 2 asubuhi nilikuwa ofisini kwa mkuu wa mkoa. Wakaongelea masuala mengine, ikafika muda wakaongelea suala langu.

Alice Haule akionyesha hati ya kiwanja alichokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila baada ya kamati kuwasilisha uchunguzi wake leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025.

“Nilishindwa kujizuia, nimelia sana, maana jambo hili limenibadilisha hadi kiafya. Limenisumbua kwa muda mrefu, lakini Mungu wetu ni Mungu wa haki,” amesema Alice, ambaye amewashukuru wote waliokuwa naye bega kwa bega kuhakikisha anapata haki yake.

Kauli ya Chalamila

Akizungumza baada ya kumkabidhi hati Alice, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chalamila, ametoa siku tano kwa mfanyabiashara Yusufali kufika ofisini kwake baada ya kushindwa kufanya hivyo licha ya kuwasiliana naye mara kadhaa kwa simu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (kulia) akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani ofisini kwake Ilala Boma, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule.

“Natoa siku tano kwa Yusufali aje mwenyewe kwa mkuu wa mkoa. Siku ya tukio la kuondolewa kwa mabaunsa huyu mama (Alice) alikuwepo, lakini baada ya mambo kuwa magumu, Yusufali hakuonekana tena nchini,” amesema Chalamila.

Uchunguzi wa Wizara ya Ardhi

Wakati huohuo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa taarifa ya uchunguzi kuhusu mgogoro wa umiliki wa kiwanja hicho kufuatia maagizo yaliyotolewa na mkuu wa mkoa wiki mbili zilizopita.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukurani Kyando, amesema timu maalumu iliundwa kupitia nyaraka, kuhoji wahusika na kuchambua mwenendo mzima wa umiliki wa kiwanja hicho.

“Timu hiyo ilipitia kumbukumbu zote kutoka wizara, mahakamani na kwa mashahidi zaidi ya wanane waliohusika tangu mchakato wa umiliki ulipoanza mwaka 2011,” amesema Kyando.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, historia ya umiliki wa kiwanja hicho ilianza mwaka 1999, ambapo mmiliki wa kwanza alikuwa Bariki Elisante Keenja. Mwaka 2007 alikiuza kwa kampuni ya Quality Real Estate na mwaka 2008 umiliki ulihamia kwa Quality Real Estate Ltd.

Baadaye, kiwanja hicho kilihamishiwa kwa Justice Rugaibula, aliyekuwa mume wa mlalamikaji, Alice Haule. Mwaka 2011, kumbukumbu za Msajili wa Hati zinaonesha kuwa marehemu Rugaibula aliihamishia miliki hiyo kwa Mohamed Mustafa Yusufali kwa makubaliano ya mauziano ya Sh262.5 milioni.

Hata hivyo, Kyando amesema jalada la Baraza la Ardhi linaonesha kuwa kulikuwa na zuio la kisheria (caveat) lililosajiliwa Oktoba 11, 2012, na Alice Haule akihoji njama za mumewe kuuza nyumba hiyo ya ndoa bila ridhaa yake.

“Timu ya uchunguzi imebaini kuwa licha ya kuwepo kwa zuio hilo, hati ya uhamisho wa umiliki ilikuwa tayari imehamishiwa kwa jina la Yusufali tangu mwaka 2011,” amesema Kyando.

Aidha, amesema kamati hiyo imepitia kesi kadhaa zilizowahi kufunguliwa kuhusiana na mgogoro huo, ikiwamo kesi namba 208/2011 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kati ya Mohamed Yusufali dhidi ya Justice Rugaibula, na kesi namba 389/2020 katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kinondoni kati ya Yusufali dhidi ya Rugaibula na Alice Pasco Haule. Kamati ilipatiwa nakala halisi na tuzo za kesi sita ambazo waliridhiana mezani.

Pia, amesema kamati imepitia kesi namba 3143/2025 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Februari na kesi namba 224396 ya mwaka 2005.

Kyando amesema kamati imehoji mashahidi zaidi ya wanane, akiwemo mwanasheria aliyeandaa nyaraka za kukopeshana fedha na mauziano kati ya Yusufali na Rugaibula.

Amesema wakili alikiri kumfahamu mlalamikaji na kudai kuwa mumewe ndiye aliyechukua nyaraka na kwenda kumsainisha mlalamikaji, lakini yeye hajawahi kumuona akisaini nyaraka hizo.

“Shahidi anasema hajawahi kumuona mlalamikaji, Alice, akisaini sehemu yoyote ya nyaraka hizo,” amesema.

Amesema kamati pia imebaini kuwa iliingiwa mikataba miwili ya kukopeshana Sh150 milioni na mkataba wa mauziano ya Sh262.5 milioni, na mikataba hiyo ilihusisha kiwanja kimoja, kwamba asipoweza kulipa Sh150 milioni angelipa kiasi hicho.

“Kamati imebaini kuwa masuala yote ya kukopeshana hayajawahi kuripotiwa katika Wizara ya Ardhi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ilichobaini Kamati

Katika ripoti ya uchunguzi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imebainika kuwa Alice hakuwahi kutoa idhini ya kuuza nyumba iliyokuwa mali ya ndoa yake na marehemu mumewe, Rugaibula, jambo lililomsukuma kuanza kufuatilia suala hilo tangu mwaka 2012.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakili aliyeandaa nyaraka za mauziano alikiri kuwa hakuwahi kumuona Alice akisaini nyaraka ya idhini ya mwenza. Badala yake, alieleza kuwa aliandaa nyaraka hizo na kumpatia Rugaibula, ambaye baadaye alizirudisha zikiwa tayari zimesainiwa.

Aidha, kivuli cha nyaraka ya idhini ya mwenza kilichowasilishwa na wakili wa Yusufali kinaonesha kuwa kimewekewa saini ya maandishi pamoja na dole gumba, jambo lililozua utata.

Wakili aliyeandaa nyaraka hizo amekiri kwa maandishi na kwa maneno kwamba hati aliyopewa awali ilikuwa na saini ya maandishi pekee, bila alama ya dole gumba.

“Nyaraka aliyoandaa mwanasheria kuhusu mauziano kati ya Yusufali na marehemu Rugaibula ililetwa kwake ikiwa tayari imesainiwa kwa mkono,” amenukuliwa akisema Kyando.

Kwa upande mwingine, kamati ya uchunguzi imebaini kuwa hatua za kisheria hazikufuatwa wakati wa kuondolewa kwa Alice katika nyumba hiyo, kwa kuwa hakukuwa na amri yoyote ya mahakama au mamlaka husika iliyoidhinisha hatua hiyo.

Kutokana na matokeo hayo, kamati imependekeza nyumba hiyo irejeshwe kwa Alice, ambaye ndiye msimamizi wa mirathi ya marehemu Rugaibula, hadi pale mamlaka za kisheria zitakapotoa uamuzi tofauti.

Imeandikwa na Mariam Mbwana, Devotha Kihwelo na Imani Makongoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *