KATIKA vitu viwili ambavyo mashabiki wa Yanga wanavisubiri hivi sasa kutokea katika klabu hiyo, suala la kumpata mrithi wa Romain Folz limechukua nafasi kubwa kutokana na uhitaji wa kuboresha benchi la ufundi, huku uongozi ukitoa msimamo wake.

Mbali na kocha, kuna ishu ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers, baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0. Itakuwaje jijini Dar, Yanga itapindua meza na kufuzu makundi kwa msimu wa nne mfululizo wa mashindano ya CAF au hali itakuwa mbaya? Ngoja tuone.

Yanga baada ya kutangaza kuachana na Folz, kocha aliyeiongoza timu hiyo katika mechi sita za mashindano akishinda nne, sare moja na kupoteza moja, huku akibeba Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0, kuna mchakato wa siri na haraka unafanywa na vigogo wa klabu hiyo kuziba nafasi iliyopo wazi.

Lakini wakati mchakato huo ukiendelea, kwa sasa kikosi hicho kipo chini ya Kocha Msaidizi, Patrick Mabedi, aliyetambulishwa Oktoba 13, 2025 kuchukua nafasi ya Manu Rodriguez.

Msimamo wa viongozi wa Yanga ni kusaka kocha mpya kabisa ambaye hajawahi kufundisha timu hiyo na wala sio kurudia wale waliowahi kupita jambo ambalo linazima tetesi za uwezekano wa Nasreddine Nabi na wenzake kurejea kikosini hapo.

YANG 01

Awali uongozi wa Yanga ulikuwa katika mchakato wa kumchukua Kocha wa Madagascar, Romuald Rakotondrabe ‘Roro’, lakini imebadili gia angani.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa juu wa Yanga ni kwamba klabu hiyo haitaendelea na hesabu za kumchukua Roro na mchakato huo umegeuziwa kwa kocha mpya mwingine.

Bosi mmoja wa juu ameliambia Mwanaspoti kuwa mchakato wa Roro hautaendelea kufuatia uongozi wao kuachana naye kwa sababu ambazo hata hivyo hawakutaka kuziweka wazi huku akiongeza kwamba pia hawatarudia kuchukua makocha waliopita klabuni hapo.

“Kwa sasa tunaendelea na mchakato wa kusaka kocha ambaye ataitoa Yanga hapa ilipo na kuifikisha mbali zaidi. Makocha waliopita tumeona walichokifanya, hivyo tunataka mwingine ambaye ataweka rekodi kubwa zaidi na sio kurudia kwa walewale.

YANG 02

Tunaheshimu kile walichotupatia kwa wakati wao, lakini ili kwenda mbele zaidi, basi lazima tufanye mabadiliko makubwa,” kilisema chanzo kutoka Yanga.

Mbali na Nabi ambaye aliifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023, makocha waliopita Yanga baada ya hapo mbali na Folz ni Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Miloud Hamdi.

Nabi hivi karibuni ameachana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini aliyojiunga nayo akitokea AS FAR Rabat, kabla ya hapo alikuwa anainoa Yanga kuanzia Aprili 20, 2021 hadi Juni 15, 2023.

Katika kipindi hicho, Nabi aliipa Yanga mataji mawili ya Ligi Kuu Bara (2021-2022 na 2022-2023), Kombe la FA (2021-2022 na 2022-2023), Ngao ya Jamii (2021 na 2022) na medali ya Kombe la Shirikisho Afrika mshindi wa pili msimu wa 2022-2023.

YANG 03

Pia akatwaa Tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili (2021-2022 na 2022-2023). Mafanikio hayo, yanamfanya kuwa kocha bora zaidi wa Yanga miaka ya karibuni.

Alipoondoka Nabi, ndipo Gamondi akatua Julai 11, 2023, kisha akaondoka Novemba 15, 2024.

Katika muda wake ndani ya klabu hiyo, Gamondi alishinda mataji matatu, akianza na Ligi Kuu Bara na Kombe la FA yote msimu wa 2023-2024, kisha Ngao ya Jamii kufungua msimu wa 2024-2025 ambao uliishia njiani baada ya kuondoka Novemba 2024.

Pia aliipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita takribani miaka 25. Kwa kuonyesha hakubahatisha, akarudia kufanya hivyo msimu uliofuatia 2024-2025, ingawa hakuiongoza hata mechi moja ya makundi. Akawa ameondolewa. Kwa sasa anaifundisha Singida Black Stars ya Tanzania.

YANG 04

Ramovic akabeba kijiti cha Gamondi, kuanzia Novemba 15, 2024 hadi Februari 4, 2025 na hakushinda taji lolote, akiiongoza Yanga katika mechi 13 za mashindano yote na ilishuhudiwa ikishindwa kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikimaliza nafasi ya tatu Kundi A nyuma ya Al Ahly na MC Alger. Kwa sasa yupo CR Belouizdad ya Algeria.

Hamdi ambaye kwa sasa anainoa Ismaily SC ya Misri, akamalizia kuiongoza Yanga msimu uliopita baada ya kuondoka Ramovic, akabeba mataji matatu kama Gamondi.

Kocha huyo raia wa Algeria aliyetua Yanga Februari 4, 2025 na kuondoka ulipomalizika msimu wa 2024-2025, alianza kubeba Kombe la Muungano, kisha Ligi Kuu Bara na kumalizia Kombe la FA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *