Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT–Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema silaha pekee ya kuzikabili dosari zinazojitokeza katika uchaguzi ni kujitokeza kwa wingi kupiga kura itakapofika Oktoba 29, mwaka huu.
Othman ameijenga hoja hiyo akirejea dosari zinazolalamikiwa na upinzani, yakiwemo madai ya kuibiwa kura, akisisitiza kuwa njia ya kukabili hilo ni kujitokeza kwa wingi na kupiga kura za kutosha.
Ameeleza hayo leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ole Kianga Laurent, Pemba, katika mwendelezo wa kampeni zake za lala salama.

“Wazanzibari na wana ACT–Wazalendo, jitokezeni kupiga kura mkiwa na amani pamoja na imani kuwa sisi ni washindi. Tunakwenda kuulinda ushindi wetu. Hawa, dawa yao moja tu asibakie mtu nyumbani. Maana nyongeza huwekwa katika fungu, hawa hawana fungu. Hebu niambie, kura zao ziko wapi? Mnaziona nyie au mnazisikia harufu ya kura zao? Hawa wameishia tayari,” amesema Othman.
Kabla ya kufika katika mkutano huo, Othman alizindua timu maalumu za vijana za ushindi zilizopewa jina la timu OMO, akisema hana wasiwasi kuhusu ushindi wa chama chake katika uchaguzi mkuu huo utakaofanyika Oktoba 29.
Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT–Wazalendo, amesema ameshaandaa timu ya kuunda Serikali atakayoiongoza kwa miaka mitano ijayo, itakayowahudumia Wazanzibari wote bila upendeleo.
Amesema chama chao kimefanya kampeni za kipekee, zilizojaa hoja, ukweli na matumaini, hivyo ni wakati wa kuvuna matunda ya kazi kubwa iliyofanywa ifikapo Oktoba 29 kutoka kwa wananchi.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT–Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amesema wana matumaini makubwa ya kuandika historia ya mabadiliko ifikapo Oktoba 29, mwaka huu, ndani ya Kisiwa cha Zanzibar.
“Hatuna pesa, hatuna dola, hatuna jeuri wala kiburi, lakini tunamshukuru Mungu tunaendelea kufanikiwa,” amesema Jussa, ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi ya ACT–Wazalendo Zanzibar.
Jussa amerejea kauli yake anayoitoa mara kwa mara kwenye mikutano ya hadhara, akisema wameshamaliza kampeni na ingekuwa amri yao wangefunga mchakato huo.

“Othman amefanya kampeni ya kisayansi, kunadi ilani ya ACT–Wazalendo yenye kurasa 100,” amesema.
Katika mkutano huo, Jussa amewaahidi Wazanzibari kuwa chama chao kikishika madaraka, vyombo vya habari vya umma vitatenda majukumu yake kwa weledi, ikiwemo kumwajibisha kiongozi na si kumpamba.
“Vyombo vya habari vya umma vitakuwa sauti ya umma, vitamwajibisha Othman na Serikali yake ili watekeleze mnayoyataka. Sitaki kazi yoyote Serikalini, kazi yangu itakuwa kuichunga Serikali ya Othman ili tuwe na tofauti na wenzetu,” amesema Jussa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT–Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, amesema kati ya mikutano ya majimbo 36, tayari mgombea wao wa urais ameshafanya 33.
“Tutakuwa tumebakiwa na mikutano mitatu. Kesho tutakwenda Chambani, kisha Tumbe, na tutamalizia Wete tutakapofunga dimba. Kati ya majimbo 50, Ole ni jimbo la 47, kati ya majimbo 18 ya Pemba, hili ni jimbo la 15,” amesema Shehe na kuongeza:
“Safari yetu ya kampeni ipo ukingoni, lakini tunaendelea vizuri na kumekuwa na mafanikio makubwa. Wito wangu kwa upande wa pili, wajiandae kufanya kazi na Othman. Tena ikiwezekana waanze sasa hata kumpigia simu, wajiandae kisaikolojia, wimbi hili halizuiliki.”