
Wakazi wa al-Fashir sasa wamegeukia mapango ya ardhini kujihifadhi kutokana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya madrasa, misikiti na vituo vya wakimbizi. Mji huo umekuwa ukizingirwa kwa miezi 18 na RSF, na zaidi ya watu milioni moja tayari wamekimbia. Waliobaki, takriban robo milioni, wanaishi kwa hofu ya mashambulizi au kulipiziwa kisasi iwapo mji utaanguka.
Kwa mujibu wa wakazi na picha zilizothibitishwa na Reuters, watu wengi hujificha mchana, hawawashi taa usiku, na hufanya mazishi tu alfajiri au usiku wa manane. “Tunaweza tu kuwazika watu usiku au mapema asubuhi. Hilo limekuwa jambo la kawaida,” alisema Mohyaldeen Abdallah, mwandishi wa habari wa ndani ya al-Fashir.
Daktari Ezzeldin Asow, aliyekuwa mkuu wa Hospitali ya Kusini ya al-Fashir huko Sudan, alisema mashambulizi yamewalenga hata wagonjwa. Katika shambulio moja kwenye shule ya Abu Taleb, watu 18 waliuawa, wakiwemo watoto.
Mashahidi walisema RSF haibagui kati ya raia na wanajeshi. Hata hivyo, RSF imekanusha madai hayo, ikidai maadui wake wamegeuza misikiti na hospitali kuwa kambi za kijeshi, huku jeshi la Sudan nalo likitumia droni.
Mnamo Oktoba 10–11, kituo kingine cha wakimbizi cha Dar al-Arqam kilishambuliwa mara kadhaa. Meneja wa kituo hicho, Hashim Bosh, alihesabu vifo 57 – wakiwemo watoto 17 na wachanga watatu. “Walipiga risasi moja kwa moja kwenye msikiti, mara baada ya sala ya Ijumaa,” alisema Bosh katika ujumbe wa sauti kwa Reuters.
Mashambulizi ya RSF yamesababisha visa vingi vya kiwewe
Katika video iliyothibitishwa, miili ya watu ilionekana ikitapakaa ndani ya kontena lililotumika kama hifadhi. Picha za setilaiti kutoka Maabara ya Utafiti wa Kibinadamu ya Yale, zilionyesha alama za miripuko sita kwenye majengo ya Dar al-Arqam. Mashirika ya kiraia yanasema watu takriban 30 hufa kila siku kutokana na njaa, magonjwa na mashambulizi. Mohamed Khamis, ni mkaazi wa kambi iliyolengwa katika mashambulizi ya RSF
“Hii ndiyo hali ya watu waliokosa makazi yao, hiki ndiyo kituo cha hifadhi ya waliokosa makazi, watu wasio na silaha, wote ni wazee na watoto waliolengwa na droni za RSF, maroketi sita. Hizi ndiyo nyumba zao, nyumba za waliokosa makazi na sas ani mashahidi chini ya vitanda na juu ya vitanda.”
Mkurugenzi wa kanda wa Shirika la afya duniani anaeshughulikia masuala ya dharura Annette Heinzelmann anasema mashambulizi ya RSF yamesababisha visa vingi vya kiwewe.
“Tangu kuanza kwa mzozo huu, kumekuwa na zaidi ya visa 15,000 vya kiwewe. Na mfano wa karibuni zaidi, katika wiki ya tarehe 14 Septemba, kulikuwa na karibu wagonjwa 500 wa kiwewe waliohitaji matibabu mjini al-Fashir.”
Wakati hayo yakijiri, kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan amesema yuko tayari kwa mazungumzo iwapo RSF itasalimisha silaha. Akiunga mkono juhudi za kundi la mataifa ya Marekani, Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, alisisitiza kuwa amani haiwezi kulazimishwa. Hata hivyo, mapigano yameendelea, jeshi likiripotiwa kuua watu saba katika mashambulizi ya ndege Darfur Kaskazini, huku hofu ya mauaji ya halaiki ikiongezeka.