
Rais Ruto amemuelezea marehemu Raila kama mzalendo shupavu, kiongozi jasiri, na shujaa wa vizazi vyote, akisisitiza kwamba maisha na maono yake yameacha alama isiyofutika katika historia ya taifa. Rais alitenga muda wa ukimya wa kitaifa kuenzi maisha ya Raila, akisema kuwa ni kwake ndipo taifa linapata msukumo wa kuendelea kupigania haki, amani na umoja.
Ruto amesema Raila alionesha kwa matendo kwamba upendo wa kweli kwa nchi unazidi maslahi binafsi,akimkumbuka kama mtu aliyekuwa tayari kushirikiana na wapinzani wake kwa ajili ya utulivu wa taifa.
“Tunapotoka kwenye juma lenye majonzi makuu na taifa linapoendelea kuomboleza kwa siku saba kifo cha aliyekuwa Waziri mkuu Raila Odinga, ni busara tunapoadhimisha siku kuu ya mashujaa kutafakari maisha ya shujaa Raila Odinga.”
Ruto asema utawala wake utapambana na siasa za kikabila
Aidha Rais Ruto aliapa kuwa utawala wake utakabiliana na siasa za ukabila, ubaguzi na migawanyiko ili kufungua njia ya kupatikana usawa katika utekelazaji wa mipango na miradi ya maendeleo. Kwa upande wake, Rais wa Senegal aliyekuwa mgeni mwalikwa, Bassirou Diomaye Faye, amewataka Waafrika wakumbatie tamaduni ya kuwaenzi mashujaa wao ili kurejesha historia ya bara hilo.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuanzisha vituo vya nyaraka na kumbukumbu kwa ajili ya kuhifadhi taarifa, ushuhuda na simulizi kuhusu mashujaa wa Afrika, sambamba na kuendeleza elimu kuhusu wapigania uhuru waliopinga ukoloni kwa ujasiri.
“Mashujaa wetu wanastahili heshima zetu zote, wanastahili upendo wetu, maisha ya mashujaa wa kenya waliojitoa mhanga, kwa kupigania uhuru wa taifa lao ni sifa kuu, na yanastahili kuonewa Fahari.”
Wazo latolewa la kuzipa barabara na majengo majina ya mashujaa
Rais huyo pia alisisitiza haja ya kuzipa barabara na majengo majina ya mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika kupigania haki na uhuru wa wananchi. Aidha, amesisitiza kwamba historia ya Afrika inapaswa kufundishwa katika mitaala ya shule nchini Kenya na barani kote, ili watoto wa kizazi kijacho wakue wakiwa na uelewa wa matukio muhimu ya kihistoria yaliyounda bara lao.
Waziri Mkuu wa Msumbiji Maria Benvinda Levi, alimwakilisha Rais wa taifa hilo Daniel Chapo huku akitaja kifo cha Raila OdingaKuwa pigo sio tu kwa Kenya bali Afrika nzima.
“Ama kwa hakika Kenya na Afrika nzima imepoteza mzalendo wa kweli, ambaye sauti yake ya kupigana kuleta ukombozi itaendelea kusika kwa jamii yenye haki na demokrasia.”
Siku kuu ya Mashujaa nchini Kenya huadhimishwa kila tarehe 20 mwezi Oktoba kuwakumbuka mashujaa walioiletea nchi uhuru lakini pia Wakenya ambao wametoa mchango mkubwa kwenye nyanja mbali mbali.