Mkuranga. Ili kupunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Kilwa (Kongowe hadi Mkuranga), mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuangalia uwezekano wa kufanya upanuzi wa barabara hiyo ili kuboresha usafiri na usafirishaji na kurahisisha shughuli za kiuchumi.
Aidha, ameahidi akipewa ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo miradi mingine yenye umuhimu kwa Wilaya ya Mkuranga itakayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara ya Mkuranga mjini hadi Kisiju yenye urefu wa kilomita 40.
Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa ahadi hizo leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mgombea huyo amemtaka Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuangalia namna ya kupanua barabara hiyo.
“Natambua msongamano mkubwa uliopo wa magari Barabara ya Kilwa hasa kipande cha kutoka Kongowe hadi Mkuranga, hali hii inachangia ucheleweshaji wa shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria, hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi,” amesema na kuongeza:
“Tunaangalia uwezekano wa kufanya upanuzi wa barabara hii, na kwa sababu wana Mkuranga mmenipa jembe (Ulega) na nimelikabidhi Wizara ya Ujenzi yeye atapekuapekua aone nini kinaweza kufanyika.”

Kuhusu miradi mingine yenye umuhimu kwa wilaya hiyo, Samia amesema ilani ya CCM ya mwaka 2025/30 imeainisha Barabara ya Mkuranga Mjini hadi Kisiju yenye urefu kilomita 40 na wataenda kuifanyia kazi.
“Inamaanisha barabara ikifika Kisiju tumefungua bandari ya Kisiju. Stendi ya mabasi sasa hili nalo tumejumuisha kwenye ilani na tunakwenda kutekeleza mradi huu, na uzuri zaidi ni kwamba wana Mkuranga mmeonyesha utayari na uhitaji wa mradi huu na tayari mmetoa eneo kurahisisha hili,” amesema Samia.
Kuhusu utoaji ruzuku amesema unaongeza uzalishaji wa mazao na kuwa nchi za Ulaya zinatoa ruzuku kubwa kwa wakulima wao na kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku na mahindi barani Afrika.
“Tanzania tulifanya uamuzi wa kutoa ruzuku kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na maeneo mengine na matokeo yake mazao ni mengi tunajitosheleza kwa chakula Tanzania kwa asilimia 128 tuna chakula cha kutosha na kuuza kwa wenzetu,” ameongeza Samia.

Kwa upande wake, Ulega amebainisha kuwa kati ya mwaka 2021 hadi 2025 jumla ya kilomita 1,384 za barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami nchi nzima pamoja na madaraja makubwa 12 yakiwamo ya Kigongo – Busisi, Tanzanite na Daraja la Gerezani Kariakoo.
Kuhusu fursa za uwekezaji katika Wilaya ya Mkuranga, Ulega amesema wilaya hiyo ina idadi ya watu 534,000 ambapo kati ya vijiji vyenye watu wengi ni pamoja na Mwandege, Kisemvule, Mlamleni na Vikindu.
“Watu hawa wamefuata fursa za kiuchumi katika wilaya yetu, kwa sababu mwaka 2021 wakati unaingia madarakani, Mkuranga ilikuwa na viwanda 214 tu. Pamoja na mdororo wa uchumi kwa ugonjwa wa Uviko-19 kwa uhusiano mwema ulioweka, wawekezaji walikuja Tanzania wakaja Mkuranga sasa vimejengwa viwanda 60 vipya, na kufanya tuwe na jumla ya viwanda 274,” amesema Ulega.
“Hata viwanda vinne vikubwa vya kubangua korosho nchini vipo Mkuranga. Haya hayakutokea kwa bahati mbaya, ni kwa ushujaa wako kwa uzalendo wako ndio maana tumepata maendeleo makubwa,” amesema Ulega.

Kuhusu sekta ya elimu, mgombea huyo amesema miaka minne wakati Samia anaingia madarakani, wilaya hiyo ilikuwa na shule za msingi 130, kwa sasa zipo 169 huku za sekondari zikiongezeka na kufika 39 kutoka 26 zilizokuwepo awali.
“Hapa Mwandege hapakuwa na shule hata moja ya sekondari lakini sasa hivi zipo tatu. Katika miaka minne umejenga zahanati 33. Upatikanaji huduma za maji kwa vijiji ilikuwa asilimia 70, sasa hivi tumefikia asilimia 80 na mjini upatikanaji maji ni asilimia 94.
“Tunaomba barabara ya Mkuranga Mjini hadi Kisiju Pwani ili kwenda kuufungua utalii,” ameomba Ulega.